Wanakwenda wapi Watoto wa vituoni?
Na Mobini
Sarya
SWALI ambalo pengine
msomaji umewahi kujiuliza ni kwamba;je wanakwenda wapi wale watoto
wanaolelewa kwenye vituo maalum wanapofikisha umri wa miaka 18?.
Wakati mwingine vinajulikana kama vituo vya watoto
yatima au vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Hilo ni swali ambalo nimekuwa nikijiuliza kama
ambavyo pengine na wewe umewahi kujiuliza lakini sasa linaweza kuwa limepata majawabu.
BCDSA tz,mkurugenzi wake, Mathew Shadrack anasema kuwa tangu kianzishwe Mwaka 2004,hawajapokea watoto wengine.
Nimekwenda vituo vitatu tofauti vya kulelea watoto
hao, viwili vipo jijini Mwanza na kimoja cha KIWOHEDE Dar es Salaam, baada ya
kuzungumza na walezi au wasimamizi wa vituo hivyo nimegundua mambo kadhaa.
Katika kituo cha Upendo Daima kilichopo jirani na
chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine,eneo la Malimbe Mwanza nakutana na Bi. Irine
Kimaro ambaye ni msaidizi wa kituo hicho.
Katika mazungumzo yangu naye nagundua kuwa kituo
hicho kilianza miaka ya 90, kilianzishwa na masisita wa kanisa Katoliki kwa
lengo la kukusanya watoto wanaoishi mitaani na kwarejesha katika familia zao.
Hiyo ndiyo
falsafa ya kuanzisha vituo hivyo, kwamba siyo mpango wala nia ya serikali
kuruhusu watu kutunza watoto katika vituo hivyo badala yake wanapaswa
kuwakusanya na kuwarejesha makwao.
Masista hao walianzisha kituo kilichokuwa kinaitwa
Day Care Centre ambapo walikuwa wanawatunza watoto kabla ya kuwarejesha makwao.
Hata hivyo baada ya ongezeko la watoto walianzisha kituo
kingine ambacho kinaitwa Back to home hiki kituo kazi yake ni eneo la kungojea
usafiri wa kuwapeleka watoto kwao mara baada ya kuwa wamejulikana wanapotoke.
“Sio lengo la kituo kulea watoto hapa, hiki kituo
kilianzishwa kwa lengo la kuwakusanya watoto wanaotangatanga mitaani na
kuwarejesha katika familia zao”anasema Bi.Kimaro
Hata hivyo hivi sasa kituo hicho kimelazimika kujipa
jukumu la kuwalea na kuwasomesha baadhi ya watoto kutokana na kwamba wamegoma
kurejea makwao.
Swali la
kujiuliza ni kwanini watoto hawataki kurejea majumbani kwao hata pale
wanapoambiwa watasafirishwa kwa gharama za vituo?
Mmoja
wa maafisa wanaofanyaka kazi ya kupeleka watoto majumbani kutoka kituo hicho Bw. Waryoba Nyamsenda anasema wanapowapata
watoto wanaoishi mitaani huwarejesha nyumbani kwao na huwapatia shilingi 50,000
kama pesa ya kununua vifaa vya shule.
“Kwanza mtoto
unakuta anafanya kosa halafu anakimbia kuogopa kuchapwa, pili migogoro ya
kifamilia inayofanya mtoto kukosa malezi, tatu njaa inayokabili familia nyingi
watoto wanamua kwenda kujitafutia au wanatumwa na wazazi wao”anasema mfanyakazi
huyo.
“Unakuta mtoto anakwambia kuwa kwetu ni Shinyanga
mnakata tiketi ya watu wawili kwenda huko, mkifika anawageuka tena anawambia kuwa kwetu ni Mara sio hapa hata jina anadanganya”anasema
Bi. Kimaro.
Bi.Kimaro anasema kuwa watoto wanaokaa nao kituoni
ni wale ambao wanagundua kuwa hata wakirejea majumbani kwao hawawezi kuendelea
na masomo kutokana na umasikini au njaa kwenye familia zao.
Bi.Kimaro alisema wamepata barua kutoka Ustawi wa Jamii,
hivyo tukiwapata mitaani wakifika hapa tunawapima uwezo wao kielimu halafu tunakwenda
kuwaombea nafasi ya kusoma katika shule ya msingi Nyamalango”anasema Bi.Kimaro
tangu waanzishe mpango huo miaka michache
iliyopita wamefanikiwa kusomesha watoto
48 ingawa kituo kinauwezo wa kuwalaza watoto 50.
Mwandishi wa
makala hii alipotaka taarifa zaidi ya idadi ya wanaosoma, alipatiwa kama ifuatavyo: darasa la kwanza watatu, la
pili watatu, darasa la tano wanne, walioingia darasa la saba Mwaka huu saba.
“waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2013
walikuwa watatu na wamefaulu wote kwenda shule ya upili (sekondari) lakini tunawachukua
watoto wa kiume tu, kuanzia miaka 6 hadi 16” anasema Bi.Kimaro.
Hata hivyo kuna watoto wawili waliokuwa wanasoma shule
ya upili (sekondari) Kilango iliyopo wilayani Magu, wameacha masomo wakiwa
kidato cha kwanza mwaka jana bila sababu hivyo kituo kimejitoa kuendelea
kuwahudumia.
Wapo wale waliohitimu kidato cha tano Nyamilama
Sekondari mwaka jana ambao ni watatu, wanaomaliza shule ya msingi wakashindwa
kuendelea kidato cha kwanza hupelekwa katika vyuo vya elimu ya ufundi.
Kituo hicho kinao watoto wawili wenye vipaji vya
mpira ambao wamechaguliwa kwenye mashindano ya kombe la dunia la watoto
wanaoishi katika mazingira magumu nchini Brazili, mwaka huu wakitoka gereji wanakwenda
kufanya mazoezi ya mpira wa miguu, nao ni Maganga Khamis (14) na Majuto
Madirisha (14).
Kituo hicho kimeendelea kuwasaidia watoto hao kusoma
kadri wanavyoweza na tayari mmoja wao amefika chuo cha sanaa Bagamoyo
(TASUBA)ambaye ni Bw.Agoustine Mgendi anasomea muziki na ngoma za asili.
“Kama unavyofahamu sio lengo letu kukaa na watoto
kituoni hata wale wanaosoma ambapo hulazimika kuishi kituoni, wanapofunga shule
huwapeleka likizo majumbani kwao, baadaye kabla ya likizo huwa
tunakutana nao mitaani wakizurura”anasema mlezi huyo.

