Friday, March 16, 2007

SHERIA HUTUNGWA NA BINADAMU,HAKI IKO WAPI

HAKI

Na Mobini Sarya

SHERIA za nchi Zimedharauliwa, Mahakama Kuu imebakwa na Nchi imevuliwa nguo na kubaki uchi huku utawala wa Sheria ukibaki na Aibu kubwa isiyostiriwa na iliyoweka historia katika Taifa letu, huku watawala wakibaki na kigugumizi wasipate la kujibu baada ya kuonekana mtunga Sheria Ndio Mvunja sheria.

Hayo matukio yote yamekuja Baada ya aliyekuwa kiongozi wa Umma Kushitakiwa kwa Kosa la kuuwa kisha kuachiwa kwa Dhamana ndani ya Siku 120 kwa madai kuwa aliuwa bila kukusudia na kuwaacha watu wakijiuliza maswali mengi kuhusu jinsi kiongozi huyu alivyoshughulikiwa haraka na kutoka kama kweli taratibu zilifuatwa.

Aibu imekuwa kubwa Zaidi na isiyofutika baada ya Kiongozi huyo aliyewahi kuwa Mbunge na Mtunga sheria za nchi kupitia Jimbo la Ilala na Baadaye kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora ,Ukiwaona Ditopile Mzuzuri kupitishwa kwenye Mlango wa Majaji wakati anaingizwa Mahakama Kuu kupewa Dhamana kitu ambacho hakijawahi kutokea huku akipewa ulinzi sawa na Rais.

Katika kuonyeha kuwa Mtunga sheria Ndio Mvunja Sheria na Sheria za hapa Tanzania hutungiwa wendawazimu tu wenyekili wakizivunja, ndugu wa Mtuhumiwa wa Mauwaji waliwageuza waandishi wa Habari waliokuwa wanafuatilia kesi hiyo kuwa ndio watuhumiwa na kuwaanza kuwaadhibu mithili ya vibaka huku wakisaidiana na Jeshi la Polisi.

matukio hayo waliyafanya sio mara yao ya kwanza ilikuwa ni kuendeleza ufedhuli waliokuwa wameanza nao tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, pale walipoanza kuwazuia waandishi wa Habari wasifanye kazi zao,kwa kuwatukana na kuwa mwagia Maji ya Upupu , na siku zingine kumfunika mtuhumiwa kanga au kumletea kofia aina ya Pama ili ajifunike kuepuka aibu ya jamii, baada ya kumuuwa Dereva wa Daladala Hassan Mbonde kwa kumtwanga na Risasi kichwani.

Katika kesi hii inayomkabili kiongozi wa Umma tusingependa kuijadili kutokana na kuwa ipo Mahakamani lakini jinsi mwenendo wake unavyokwenda na matukio yaliyoambatana nayo hiyo kesi hakuna kizuizi chochote kinachoweza kuzuia isiandikwe wala kuzungumzwa mitaani, kwani hadi sasa kila mmoja anayeifutalia anajua kinachofanyika au kuendelea.

Katika mwendendo mzima wa kesi umekuwa ukiacha Maswali mengi kuliko majibu kila kukicha huku Haki na Sheria vikikiukwa kwa uwazi bila kuhojiwa na hali ilianza kushangaza katika Mahakama ya Kisutu pale Ndugu zake na Ditopile walipofanikiwa kumfunika kanga ili asipigwe picha huku Polisi wakichekelea, Maswali yaliyoibuka hapa ni kwamba ndugu zake walipataje nafasi ya kumkaribia Mtuhumiwa wa Mauwaji kiasi hicho ikiwa Mahabusu wa kawaida tu ndugu zao wanazuiliwa kuwasogelea pale wanapofikishwa Mahakamani.

Je katika hili Polisi walikuwa wanajua wajibu wao kwa kuwaruhusu Ndugu wa Mtuhumiwa wa Mauwaji kumsogelea,wangewezaje kumzuia mtu mwingine ambaye angejipenyeza kama ndugu wa Mtuhumiwa kumbe akiwa na Lengo la kumchoma kisu Mtuhumiwa, ilikuwaje Polisi katika Mahakama ya Kisutu waendele kuwashuhudiwa ndugu wa Mtuhumiwa wakiwafanyia wandishi vitendo vya Dharau hadi pale Hakimu alipoingilia kati na kusema wazi kuwa Polisi walikuwa wamezembea kupita kiasi?


Kama kuna mkono wa Mtu unatumika katika Kesi hii basi ulianza kutumika kikamilifu katika Mahakama ya Kisutu na Polisi walilishwa Limbwata wakawa kama Chatu aliyemeza Mzoga na kulala asijue la kufanya huku wakiangalia vitendo vya uvunjwaji wa sheria za nchi.

Kama hiyo haitoshi inafahamika Wazi kuwa mbele ya Pesa hakuna kinachoshindikana kwa Polisi, hali ilikuwa mbaya zaidi walipomfikishaMahakama Kuu kwani waliamua kunajisi Mlango wa Majaji wanaotumia kupitia au kutokea Makakamani kwa kumpitisha Mtuhumiwa, wakati wanajua kuwa huo Mlango hata Mfanyakazi wa Mahakama hiyo Haruhusiwi kuupita ,mlinzi wa Mahakama alipojaribu kuuwazuia wakamnyanyasa kwa kusukuma, hadi wakafanikiwa kutizima Azima yao..

Kitendo kilichowakasilisha Majaji wa Mahakama hiyo na kuamua kumtaka Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Alfred Tibaigana atoe Maelezo,ndani ya Muda ambao Mtuhumiwa alipewa Dhamana katika Mahakama Kuu hiyo ndugu zake waligeuza eneo hilo kuwa uwanja wa Masumbwi kwa kuwaadhibu waandishi mbele ya Mahakama ya Haki huku wakiimba kuwa nchi hii ni yao kama wandishi walikuwa hawawajui watajua sasa, nakuwajeruhi wandishi Kadhaa.

Baada ya kuangalia Mwenedo mzima wa hii kesi wananchi wameingiwa na hofu kama kweli Hapa haki itatendeka jinsi inavyopelewa, toka Mtuhumiwa alipokamatwa amekuwa akihusishwa Mojakwamoja na Utawala wa Serikali ya Awamu ya nne kitu ambacho kimethibitishwa na Ndugu wa Mtuhumiwa Mahakamani walipokuwa wanapigwa watu huku wakijitapa kuwa nchi hii ni ya kwao, kweli Polisi wakawa wanawaunga Mkono.

Siku chache tu baada ya Ditopile kushikiliwa na Polisi kwa Kuuwa Dereva Novemba 8 Mwaka jana, baadhi ya vyombo vya Habari viriripoti kuwa Rais Kikwete amekiri kuwa Dito alikuwa Mwanamtandao wa kuaminika, amesononeshwa na tukio hilo hajui afanye nini,akasema anaachia Sheria ifanye kazi yake.

kutokana na Tanzania kuwa mfumo Mbaya wa Sheria za Kulindana kumesababisha mtuhumiwa wa Muwaji kubadilishiwa kesi nje ya Mahakama Kuu kupitia Dirishana laa nyum na kuwa kesi ya kuuwa bila kukusudia kwa muda wa siku 120 tu.

Huku watu waliokamatwa kwa kuhisiwa tu wengine na makosa madogomadogo wamesota Jela na wengine kufia Mahabusu bila Kesi yao kusikilizwa wakiambiwa kuwa upepelezi bado haujakamilika, na kunyimwa Dhamana bila maelezo ya msingi huku wakinyimwa nafasi ya kuonana na ndugu zao,wapo wanaolalamika kunyimwa huduma ya matibabu kutoka kwa ndugu zao.

Kuachiwa kwa dhamana Mtuhumiwa wa Mauwaji kwa upande wa Pili kumefungua njia ya Ukombozi na Mapinduzi kutokea Magereza,tukio hilo limehitimisha yale manung’uniko ya Muda mrefu kuwa magereza Tanzania ni sehemu ya kuwatunzia walalahoi huku wenye nguvu wakiachiwa bila kutiwa hatiani hata kama kuna ushahidi wa wazi kuwa mtuhumiwa alitenda kosa kwa kukusudia.

Hapa Tanzania imekuwa ni Kawaida Tajiri akiuwa anaambiwa kajeruhi lakini Mlalahoi akijeruhi anaambiwa kauwa, kibaka anauwawa, Mzururaji anaandikiwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia Silaha na kunyimwa dhamana wengine kubambikiziwa kesi wasiozijua huku wakiambulia kipigo cha maumivu ili wakubali kosa ambalo hawakulitenda.

Mgomo wa Siku kadhaa wa Mahabusu uliotawala katika Magereza ya maeneo mbalimbali hapa nchini, umeashiria Mwanzo Mpya wa Mapinduzi ya haki na ni Mwanzo wa aibu kubwa kwa Taifa kama letu linalojivunia Utawala bora wa Sheria na kulinda haki za Binadamu.

Wiki nzima iliyopita imegubikwa na aibu kubwa kwa Taifa, Mahabusu wakitaka haki ambayo wameikosa siku Nyingi wapo waliokamatwa kwa kuiba kuku wamekaa Rumande kwa muda mrefu wakiambiwa upelelezi bado haujakamilika, lakini wengine wanakamatwa kesho yake kwa Mauwaji au kulawiti watoto wanadhaminiwa.

Wikii hii tumesikia katika Gereza la Isangu Dodoma wafungwa waliokamatwa kwa kosa unyang’anyi baada ya kukaa rumande bila dhamana sasa wamebadilishiwaa kesi ya kuua na kule Serengeti Polisi walikamata Madumu ya maji wakazani ni mafuta ya Disel wakambambikizia mwananchi mmoja wakakaa naye kituo kikuu toka asubuhi hadi jioni bila dhamana wakitaka rushwa hadi mwenye madumu alivyjitokeza jioni nakuomba madumu yake Polisi wakashtuka kumbe ndani kulikuwa na maji.

Kesi hii ya Ditopile imetufanya tufahamu kuwa kumbe kuna wananchi na Walanchi tumefahamu kwamba kuna watu wameuwa lakini hata mahabusu wengine hawakufika miongoni mwao ni aliyekuwa mkuu wa Upelelezi Mkoani Dar es Salaam( RCO)Abdallah Zombe upelelezi wake ulikamilika ndani ya siku 150 yeye yupo rumande,

Mtoto wa Balozi Rupia aliyetuhumiwa kwa kosa la Mauwaji na kuachiwa baada ya siku tisa , Mtoto wa Kingunge ambaye hata hakufika Mahakamani na Mtoto wa Sumaye naye alituhumiwa kwa mauwaji lakini wote hawa wanatesa uraiani.

Kutokana na Mwenendo usio faa wa kuendesha kesi hapa nchini wananchi wote wanapaswa kuungana kupinga haki kutolewa kwa kubaguana, pia tunapaswa kuungana na Mwanaharakati Cristopher Mtikila kuiomba Mahama kufuta Nafasi ya Mwendesha Mashita wa Serikali kwa ni tumegundua wazi kuwa nafasi hiyo ipo kwa ajili ya wakulinda vigogo wachafu, kama kunasheria mbaya ya nchi hii inapaswa kulaaniwa ni sheria inayomtambua Mwendesha Mashitaka (DPP)

Mwendesha ni mtu anayebaka haki za Majaji kutokana na kupewa uwezo wa kuruhu kesi iende Mahakamani au isiende na kupewa uwezo wa kuibadili kama anavyovyopenda na hii nafasi ilianzishwa na Wakoloni wakati ule Ili kujilinda dhidi na Ufedhuli waliokuwa wanawafanya waafrika, hata walipokabidhi Madaraka wamewaachia watawala wetu ndio wanaitumia kujilinda wakituhumiwa kuwa wamekula Rushwa wanamkimbilia Mwendesha mashitaka anawabadilishia kesi.

Mwendesha Mashtika anaingilia uhuru wa Mahakama na kuwafanya Majaji wawe vibaraka wake kama yeye alivyo kibaraka cha viongozi wa Serikali ,haiwezikani abadilishe Mashitaka yawe ya kuuwa Bila kukusudia nje ya Mahakama halafu anawapelekea Majaji wa Mahakama Kuu wagonge Mhuri wa kumpa Dhamana Mtuhumiwa bila kuona kesi yake kwanza kama ni hivyo basi hata Dhamana angetoa yeye.

Sheria hii anayoitumia DPP anaitumia kwa wananchi wote kusingekuwepo na msongamano wa wananchi mahabusu kwani wengi wametenda makosa bila kukukusudia, tangu wandishi wamepigwa na kuharibiwa vifaa vyao Polisi wameshindwa kuwachukulia hatua wale waliohusika, kitu kinachotushawishi tuamini kuwa lile tukio liliratibiwa kikamilifu na Polisi.

Kesi hii imetufundisha Mambo mengi imetuonyesha jinsi ndugu wa Watawala wanavyotenda makosa kwa makusudi wakitegemea kuwa watasaidiwa na wakubwa wao, na jinsi walivyoweza kuidhalalisha serikali ambayo imechaguliwa na wananchi,lakini hii hatavumilika siku zote, waandishi wameonyesha nia ya Mapambano pia Mahabusu wamebipu tunawasubiri wananchi waungane na wanaharakakati kufanya Maadamano ya kupinga kubaguliwa wanyonge na kukandamizwa haki zao.

Wiki ijayo nitaeleza jinsi mwendo mbaya huu wa kesi ulivyoanza kujionyesha kuwa Mnyonge hana Haki nitaonyesha jinsi Kiongozi wa Nchi anavyotakiwa awe, asiyekuwa na ubiwa na mtu kwenye madaraka yake
Kwa Mara ya kwanza historia ya Taifa letu imetiwa doa kubwa na viongozi wenyewe serikalini,watuhumiwa wahukumiwe kulingana na sheria sio utashi wetu kisiasa!!!!!


Web.www.mobinday.blogspot.com email.mobinsons@yahoo.com

Thursday, March 15, 2007

TASISI YA VYOMBO VYA HABARI YAANZISHA TUZO

TAASISI ya vyombo vya habari vilivyo kusini mwa Afrika (MISA- Tan) imeandaa tuzo ya kuzuia rushwa (Anti - Corruption)kwa waandishi wa habari watakaoandika makala zenye ubora na ubunifu.

Tuzo hizo ambazo zinashindanisha waandishi wazoefu wa magazeti, Luninga na Redio lazima washiriki wake wawe wametumia lugha ya kiingereza na kiswahili kwa kuwa ndio lugha inayosomwa na watu wengi na mshiriki anaweza akaingia kwenye shindano na makala zaidi ya moja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa( MISA -Tan) Ayoub Rioba alisema kuwa tuzo hizo zitakuwa kwa washindi watatu ambapo mshindi wa kwanza atapata dola za kimarekani 2000, mshindi wa pili dola za kimarekani 1000 wakati mshindi wa tatu dola za kimarekani 500.

Alisema kuwa kuna taratibu ambazo zitapitiwa mpaka mshindi apatikane ikiwa ni pamoja na makala lazima iwe yako pamoja na ubunifu wa kazi pia utaangaliwa.

" Ili mshindi apatikane lazima tuangalie makala hii imeandikwa bila kuwekwa utashi wowote na je itatusaidiaje sisi kupiga vita Rushwa, na lazima iwe inahusu vitu vya hapa Tanzania" alisema Rioba.

Rioba alisema kazi za washiriki zinaanza kupokelewa leo hadi Agosti 25 ambapo washindi watatangazwa Septemba mwaka huu.

Alisema wameamua kuandaa tuzo hiyo kutokana na ufadhili walioupata kutoka USA na kutakuwa shughuli mbalimbali pamoja na mafunzo ya uandishi.
MWISHO.

AFRIKA INAKWENDA KUJIFUNZA NINI ULAYA?




Na Mwandishi Wetu

AFRIKA kumepambazuka, viongozi na wanasiasa wakiafrika, wameamka wanapishana kwenye viwanja vya ndege wanawahi ulaya, wanakofikiri ndipo kuna Elimu bora ya uongonzi wenye nguvu na uhakika wa kudumu madarakani.

Wanasiasa wanawahi ulaya kujivunza mbinu za kuingia Ikulu kwa kupandikiza chuki kwa wananchi ili wazione serikali zilizopo madarakani hazifai, viongozi wa kiafrika nao wanadhani Ulaya ndipo kuna mwanga bora wa kujifunza namna ya kudumu madarakani kwa miaka mingi bila misukosuko.

Kwa maana nyingi wanasiasa wa kiafrika wanaamini kuwa Ulaya na Nchi za Magharibi ndipo kuna mzimu wao wa kuaminika bila kwenda kutambika huko na kukubaliwa hawezi kuwa kiongozi hata ikitokea akachaguliwa na wananchi bado anaona uongozi wake hauwezi kudumu kama Nchi za Magharibi hazijamkubali.

Wamekuwa wakiamini hivyo na ndivyo wanavyoamini kutokana na akili zao na hata wazungu walishawajua kuwa kiongozi wa kiafrika bila kufuta Baraka ulaya hajajiamini kabisa kuwa yupo madarakani na vilele wanasiasa wanaojiandaa kuingia Ikulu bila kwenda Ulaya kupewa somo bado hajajiamini.

Viogozi na wanasiasa wakiafrika hawataki kabisa na wala hawana muda wa kukaa chini na wasomi wao wakajidiliana sababu ya Afrika kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo hadi sasa Miaka 50 baada ya Vuguvugu la Uhuru, wala hawataki kujifunza namna na kutumia Raslimali zilizopo kuletea mataifa yao maendeleo.

Ubinafsi na uchoyo na kuendelea kuimba kuwa sisi Afrika ni maskini ndio tabia nyingi za viongozi wa Afrika wamezoea kuomba lakini hawataki kujifunza namna ya kuepuka tabia za kuomba omba.

Hali hiyo ndiyo inayochangia tuendelee kubaki nyuma kimaendeo kama hapa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete Tangu amechaguliwa Disemba 2005,Muda mwingi amekuwa akiutumia kuwaza safari za ulaya kuliko kufikiria namna ya kuwaletea wananchi wake Maendeo na Taifa kwa ujumla.

Kumbukumbu zianaonyesha kuwa Rais Kikwete amekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kutumia muda mwingi wa kufanya ziara kila pembe ya Dunia kuliko Rais Mwingine, pia hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kuwa tangu Kikwete achaguliwa amekwisha fanya ziara ya nchi nzima kwa ajilim ya kuwashukuru wananchi baada ya kumchagua.

Rais kikwete wakati anafanya kampeni ya kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya nne wa Tanzania alikuwa na kauli mbiu yake maarufu ya Maisha Bora kwa kila Mtanzania yanawezekana kauli mbiu hiyo ilimsaidia sana kuvuna kura nyingi za walalahoi.

Leo ni Mwaka mmoja na miezi mitatu imekwishatimia tangu Kikwete akabidhiwe funguo za Ikulu ,bado maisha bora kwa watanzania yamebaki kuwa ndoto Rais haonekani kila leo wananchi wanaambiwa amekwenda ziara nje,Amerika na Ulaya sasa imekuwa kama Chimwaga ya Dodoma.

Wananchi wakihoji kwa nini Rais asikae fikirie kisha ajadiliane na wataalam, namna ya kutumia raslimali zilizopo kutuletea maendelea, wasaidizi wake wanawajibu wananchi kuwa ziara zake zina mafanikio wakihojiwa hayo mafanikio wanajibu kuwa yataonekana baadaye.

Imekuwa ni kawaida kusikia wanasiasa wakijibu kwa nguvu kuwa wale wanaohoji ziara za Rais ni vipofu wasioona mafanikio yake,awali tulikuwa tunaambiwa kuwa Rais anakwenda kujitambulisha nje hoja ambayo haikutegemewa kulingana na wadhifa aliokuwa nao Kikwete kabla hajawa Rais.

Watanzania hawakutegemewa kuambiwa kwamba rais wao anakwenda kujitambulisha nje wakati waliambiwa akiwa kwenye kampeni kwamba wachamgue yeye kwani alikuwa na uzoefu wa mambo ya kimataifa baada ya kudumu wizara ya Mambo ya nje kwa kipindi chote cha serikali ya Mkapa.

Kwa hiyo ilikuwa na nafasi nzuri ya kujitaambulisha nje, hata yeye mwenyewe amekuwa akisema kuwa alianza kampeni tangu Mwaka 1995, kwa hiyo alikuwa anafanya kampeni ya kujitambulisha hadi nje kama nilivyowahi kusema kuwa hata mwanasiasa wa kiafrika anaayejiandaa kuingia Ikulu huanza kutafuta baraka nje kwanza.

Kama Kikwete anakiri kuwa aliweza kufanya kampeni kwa Miaka 10 kabla leo Amekuwa Rais tunaambiwa kuwa anajitambulisha nje,watanzania tunahitaji majibu sahihi zaidi, wala hatuwezi kuwa wepesi wa kukubali kila jambo anajitambulisha nini sasa?.

Baada ya Muda wa kujitambulisha kupita sasa tunaambiwa kuwa Rais anakwenda kutafuta Mafanikio nje, hapo ndipo yanaibuka maswali yasiyopatiwa ufumbuzi kwanini Rais atumie gharama kubwa kwenda kutafuta mafanikio nje wakati alikwisha fanya kampeni kwa miaka 10 nakujitayarisha kisha akajifunza namna ya kuwaletea wananchi maisha bora?.

Rais anakwepa majukumu yake ofisini kwani asitulie atumie maliasili zetu zilizoopo kuleta mafanikio kuliko kukimbilia nje kwenye ziara ambazo zingefanywa na Waziri wa mambo ya nje Benard Membe, ni lini nchi au Familia iliendeshwa kwa kutegemea Misaada ya kuombaomba?

Leo Tanzania inaongozwa kwa kutegemea misaada ya kuombaomba uchumi utakuwa lini,tuaweza kushindana kwenye soko la utandawazi kwa kutumia mtindo wa ombaomba,sijui kama kati ya Ilani za Uchaguzi za CCM kama kulikuwa na ilani iliyokuwa inataja kuwa Maendeleo ya nchi yatapatikana kwa kutegemea msaada wa Ombaomba.

Baada ya kuwa Rais kikwete amemaliza ziara zake hivi karibuni katika nchi za Scandnavia, ziara inayoelezwa kuwa ilikuwa ya kulipa fadhila kwa watu waliomsaidia kwenye kampeni wananchi sasa wanamtaka akae chini atafakari namna ya kuwaletea maendeleo.

Aachane na Fikra kuwa maendeleo yanapatikana kwa kuomba, inakuwa ni aibu kwa nchi kama ya kwetu iliyojaliwa utajili wa kila aina kiomgozi kukwepa majukumu ya kufikiri namna ya kutumia utajili huu ili kuinua uchumi wan chi matokeo yake anakwenda kutalii ulaya, na bahati mbaya zaidi misaada wanayopewa inakuwa sawa na chakula cha kula papohapo.
Miaka 50 ya uhuru wa Afrika lakini bado fikra hazijawaondoka viongozi wetu wanafikiri bila misada ya wazungu Afrika haiwezi kuendelea, ndio utakuta sisi tunamaliasili lakini tumeshindwa kujimalisha kwa kujenga viwanda kwa ajili ya kuzizalisha,na kuajili wafanyakazi lakini tumebaki tukizipeleka ulaya ambako hulipwa tu visenti vichache.

Angalia mfano hapa duniani Tanzania pekee imejaliwa kupata madini ya Tanzanite lakini cha ajabu viwanda vya kuyachambua na kuyatengenezea vito vipo ulaya sio kwetu Tanzania sisi tunachoambulia sio faida bali ni kodi sawa wanayolipa watalii wanaokuja kutembelea wayama, hakuna kiongozi wetu aliyewahi kuhoji hili jambo.

Ni vema sasa rais Kikwete Akakaa akatulia baada ya kujifunza atumie muda mufupi uliobakia kuwaletea wananchi maendeleo na kuachana na ziara, ambazo tunaelezwa zitakuwa na mafanikio baadaye, kwa sababu itafikia wakati viongozi wa ulaya wakisikia kionsozi wa Afrika anakwenda kufanya ziara huko wanamkacha wanajua kua anakwenda kuomba msaada.

Tumechoka kusikia kila mara kwamba nchi Fulani imetupatia msaada mbona hatuambiwa fadhila tunayowalipa baada ya kutupa huo msaada ni wajibu wetu sasa kujifunza mbinu ya kuimalisha viwanda hapa nchini ili tuweze kuvitumia kuzalisha mali na ajira kuliko kutegemea misaada, ni vizuri kuwauliza mataifa makubwa njia walizotumia wakaimarika kiuchumi kuliko kuwauliza njia na masharti ya kupata mkopo!

Ni aibu miaka 45 ya uhuru wetu leo tunaongelea tatizo la umeme na kwenda kuazima mvua za kumwagilia wakati kuna nchi kama Libya inajangwa wala haina hata bwawa lakini tatizo la umeme kwao ni hadithi sisi tunayobahari yenye mawimbi lakini tumeshindwa kuyabadili tupate umeme tunayo gesi tumeishindwa kuitumia.

Kikubwa hapa ambacho Rais Kikwete anatakiwa kutufanyia aache historia ni kutumia Madini ya Nyuklia yaliyopatika kusini Mwa Tanzania kama kigezo cha kujipatia maendeleo, watanzania tutumiea hayo madini kuwatisha mataifa makubwa ili watusaidie kupata njia za kupiga hatua ya maendeleo na kupata umeme wa uhakika wala sio kutegemea kuombaomba na kuwaombolezea.

Ni vema Rais Kikwete akakutane na wataalamu wetu azungumze nao kwa lengo la kuanza mpango wa Nyuklia ili kuwatia wasiwasi mataifa makubwa yaanze kumimina maendeleo hapa, kama walivyofanya Libya na Korea Kaskazini pia wanavyojaribu kufanya Iran, nchi hizi zote zilitishia kutumia madini ya Nyuklia kutengeneza nishati ya Ummeme hali iliyopelekea Mataifa makubwa ikiwemo Marekani kuziomba kuziapatia umeme na ahadi nyingine ili ziachane na tabia mapango huo.

Leo Tanzania tunayo Madini ya Nyuklia tukiamua kuyatumia kama silaha ya kujihami kunauhakika mkubwa kwa mataifa makubwa yatatetemeka na kutuuliza manataka nini ili muachane na biashara hii, tutawaambia,tufutieni Madeni mliyotulundikia kisha tuanataka na sisi tupige maendeleo sio kuendelea kuwaombaomba huku mkituwekea maendeleo.

Rais Kikwete sasa hivi amemaliza mwaka mmoja na miezi mitatu Ikulu amebakiwa na miaka mitatu tu Ikulu akiendelea kuitwa Rais zaidi ya hapo ataanza kuitwa Mgombea wa uRais kwa hiyo hatakuwa tena na muda wa kukaa kufikiria maendeleo bali utakuwa ni muda wa kuvaa nguo za kijani na kuanza kufanya kampeni kwa hiyo ni wajibu wake sasa kutumia miaka mitatu iliyobaki kuinua uchumi wetu unaozama.

Imesalia miaka mitatu tu ikulu kabla Kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa hazijaanza sijui mtawaeleza nini watanzania na hakuna chochote kilichofanyika wananchi wamebaki wanalia maisha magumu wameamua kuwaliwaza kwa kuwapatia mikopo inayolenga watu wa mjini kuliko wa kijijini kutokana na kwamba mikopo ni wafanyabiashara na kijijini ni wakulima na wafugaji.

mobinsons@yahoo.com 0753 399 579

huu ni utapeli wa kimataifa kwa watumiaji wa Internet

HIZI NDIO SIASA ZA KULINDANA

Wanawake



Pole sana Mama amina Chifupa hukujua Siasa yetu?

Na Mobini Sarya

Machi 8 ya kila Mwaka ni Siku ya wanawake Duniani,akinamama wengi huitumia siku hiyo kukutana na kujadiliana mambo mengi kubadilishana uzoefu wa amamboyahusuyo maendeleo yao na Maisha ya kila siku.

Lakini pamoja nakwamba siku hii inawahusu akimama wote Duniani lakini imekuwa na Nguvu sana Mjini kuliko mashambani, kwani ni mara chache sana utawakuta akimama wa vijini akiwa kwenye mikutano ya kujadiliana mambo ya maendeleo yanayowahusu, na hii inatokana na kuwepo kwa utamaduni tafauti kabisa na wa mjini.

Siku hii ya Machi 8 wanawake huitumia kudai Uhuru zaidi na Haki sawa kutoka kwa wananume kama walivyoazimia kwenye Mkutano wa wananawake Beijing China, mkutano ulioongozwa na Mtanzania Balozi Mongela, katika mkutano huo wanawake waliapa kuendeleza mapambano hadi Haki sawa Ipatikane.

Tafauti na wanawaake wa majini utamaduni wa kisasa kuwaruhusu kudai haki sawa kama walivyo wanaume lakini kwa Mwanamke wa kijini inakuwa tafauti,pamoja na mateso na manyanyaso wanayoyapata akinamama wa kijijini bado hawajaona Umhimu wa kudai haki sawa kutoka kwa mwanaume, sio kwamba hawajaelimika bali mila na desturi zao zinawafanya wawe hivyo.

Mwanamke wa mashambani anaona ni kumkosea Adabu Mme wake akimwambia wote wawe na haki sawa yaani akipika Mchana mwanaume ajiandae kupika Usiku la sivyo waende hotelini, kwani kijini hata hoteli hakuna, pia Mwanamke wa kijini anaona wenzake watamcheka ikiwa wataona mme wake anamsaidia kazi zile wanaita za kike asije akaambiwa ndio maana unamtawala mwanaume wako.

Kwa ujumla utamaduni na mazingira ya kijini ni Tafauti kabisa nay a Mjini hasa kutokana na Mazingira, shughuli zianzofanywa huko kwani ni vigumu kuwakuta akinamama kijiji wamekusanyika wanateta jambokama hilo, bila kwenda shambani, kusenya kuni ,kuchunga mifugo na kuteka maji numbali mrefu, zaidi ya hapo labda uwakute wanakusanyika kwa ajili ya kucheza upatu.

Lakini mjini kama ni siku ya wanawanawake hata ofisi sa Serikali zianfungwa kuwaruhusu waende kwenye mikutano asiye fika ataona kupitia kwenye television au kusoma Magazeti, pia kuna Tasisi nyingi mjini zinazotumika kuwahamasisha wanawake
Na kutetea haki zao ingawa zipo zingine zinafuka mipaka ya utamaduni kama chama cha wanawake waandishi wa ahabari TAMWA.

Wakati wanawake wanapokuwa wapo kwenye mapambanao ya kudai haki na usawa watukumbuke na sisi wanaume wasije wakadai haki yote tukakosa hata ile thamani ya kuitwa wanaume kwani tunajuwa sisi wanaume ni watu wenye huruma sana huwa tunajiuliza kama nyie wanawake mngepewa madaraka mkawa juu yetu ingekuwaje angalia sasa hivi wanaume wa mjini wanavyuopata shida kuliko wa kijijini.

Sio lengo langu kukwamisha juhudi mlizokwishananzisha, lakini ni bora ikaheshimiwa Misingi iliyowekwa na Mwenyezi Mungu kwa wanaume kubakia na Heshima yao na wao kuwatambua wanawake kuwa ni wasaidizi wao kuliko mwanamke kutaka kuwa na Sauti kwenye Jamii kama Mwanaume, wakati mkiendelea kusherekea mwezi huu siku yenu endelea kutafakari ni kwanini ndoa za mjini nyingi zinavunjika kuliko vijijini?

Leo sipendi kuingia ndani zaidi lakini ipo siku nitahohoji uhalali wa Hiki cha cha TAMWA kutumia pesa za Wafadhili kuharibu na kuangamiza utamaduni wa kiafrika kwa kuigilia uhuru wa watu, nawaachia swali hili, nini aliwapora wanawake haki zao tukiwa mafahali wawili kwenye zizi ndoa itadumu, tutaishije inatakiwa tafakuri.

Baada ya kuwapa Salaam akinamama leo Gumzo linamzunugumzia Mbunge wa Viti Maalum Vijana,Amina Chifupa,nampongeza mwana mama huyu kijana anayewakilisha Vijana katika Bunge la Tanzania baada ya kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi CCM, kwa sababu wiki iliyopita ilikuwa ya wanawake nimeamua kutumia Safu hii kumpongeza , kumpa Pole kisha kumpa Ushauri.

Kwanza nampongeza kwa kujipa ujasiri akajitoa Mhanga akiwa kama Mbunge mgeni bungeni akaamua kusema kwamba yupo tayari kuwataja wauza madawa ya kulevya ambao wanafahamika dhahiri kuwa ni wafanyabiashara hatari na wakubwa jijini Dar es Salaam, ambao kwao kumdhuru kiumbe yeyote alitayari kuwahatarishia biashara zao sio kazi ngumu, lakini Amina hakujali hiyo alisema kisha akarudia kusema kuwa aanawafahamu na atakuwa tayari kuwataja majina.

Alisema kwenye kikao cha kwanza Cha Bunge lakini hakuna aliyemfutilia kumuuliza ingawa mamlaka zipo na zilisikia kikao kingine kilichofuata alisema tena kwambana yupo tayari kuwata watu wanaowauzia vijana wetu madawa ya kulevya na kuwaharibu akili zao hapo pote hakuna mamlaka iliyodhubutu kupata ukweli kutoka kwake.

Pia nampa pole mbunge huyo kwa kutokuelewa siasa za Nchi yetu, Amina alikuwa Mwandishi wa habari awali alifikiri yale yaliyoko kwenye uwandishi ndio yaliyopo kwenye waheshimiwa hao alijikuta yupo katikati ya kundi la mbwa mwitu akizani kuwa yupo na kondoo, nampa pole kwa sababu yeye alipoteuliwa kuwakilisha hiyo nafasi alidhani nawote walifanya hivyo hajui wenzake walitumia hela nyingi na zingine nikutoka kwenye hayo madawa au aliwajua ndio maana wakampuuza?

Amina pamoja na kuwa anatokea Chama tawala lakini nampa Pole kuwa hajawahi kujifunza zile siasa za CCM ambazo ni kuvumiliana na kulindana kama wewe ni mwenzetu hasa ikizingatiwa kuwa mchango wako unautoa kwa moyo mmoja wakati wa uchaguzi Mkuu na unafanikisha ushindi wa kishindo leo akija mtu anakutuhumu kuwa pesa zako ni haramu hapo tutakulinda,

Kwa kutokuelewa kwake alijikuta kwenye matatizo makubwa ambayo yalitaka kumvunjia ndoa yake, nampa hongera kwa kuinusuru najua sasa amekomaa na awe tayari kuendesha mapambano kwa mazingira yoyote, ingawa aliposema anawafahamu wauza madawa na vijiwe vyao wabaya wake walinza kumponda kuwa anajitakia umaarufu, lakimi sio kweli kama ni umaarufu Amina Chifupa wa Mpakanjia aliupata akiwa Mtangazaji, hakuna mtangazaji anaye mfikia kwa umaaarufu.

Kwa hiyo yeye alikuwa amedhamiria kuwasaidia vijana anaowakikilkisha Bungeni, lakini kumbe hakujua siasa ya nchi yetu ambayo ni kulindana na ndio immefanya nchi yetu ibaki nyuma kimaendeleo mtu anaharibu wanaendelea kumkumbatia.

Lakini kwenye hili Swala la wafanyabiashara wa Madawa ya kulevya napenda kumpa Amina ushauri kuwa akae Pembeni kwani watawala hawajawa tayari kupambana nalo ache kabisa kwani hii ni biashara ya wakubwa wala sio ya watoto, wanagekuwa wanyonge na walalahoi wanahusika nayo ingekuwa imekwisha pigwa marufuku, huoni mifuko ya Rambo tunayotumia kama begi kutunzia nguo na kusafiria wameipiga marufuku sasa watakuwa wanatucheka tukishikilia nguo njiani.

Madawa ya kulevya yangekuwa ni biashara ya walalahoi, wahusika wangekuwa wameshughulikiwa kikamilifu, kama walivyofanya kwa wauza maji ya viroba wanajua sisi Maskini ndio tunaponea wameamua kuyapiga marufuku sasa tunakunywa yale wanayonawa mahotelini Afya zetu zimebaki Mashakani kipindupindu kitaisha kweli?

Biashara ya Madawa ya kulevya ni ya wakubwa na miongoni mwao wanafahamika kama alivyosema Amina lakini ninani wa kuwahoji hawa, kila mmoja anayefuatilia vyombo vya habari atakubalina nami kuwa Mwaka juzi Luten Yusuph Mkamba akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alijitosa kupambana na wauzaji wa madawa hayo alidhani kuwa ni Machinga kumbe Mh!

Makamba alitangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mwenye kufahamu wauzaji na wasafirishaji na waingizaji wa Madawa hayo nchini ampeleke majina vijana bila kujua hatari ilikuwa inawakabili walitoka hadi mbeya wakamletea maajina ya madawa hayo lakini baada ya kupewa majina hayo Makamba aligeuka Bubu hadi leo jeuri yake ya kuwashughulikia wahusika sijui iliishia wapi, sikumbuki ni wapi likini alinukuliwa akinongo’neza kuwa wenye majina yale wanamzidi hata Madaraka!!

Maajabu hayo ni watu gani hao wanaomzidi mteule na Mwakilishi wa Rais kwenye mkoa, madaraka? Je kama Makamba aliyechaguliwa na Rais ameogopa kuwashuigulikia ninani mwenye wajibu huo, kikosi cha kupambana na biashara hii kazi yake ni kukamata wale vijana wanaohusika kuyauza na wala sio wale wanaowatuma au kutuhumiwa? Kazi ya hiki kikosi haina tafauti na TAKURU ambao ni hodari kumkamata mtendaji aliyechukua hongo y ash.500 na sio wanaotuhumiwa kula Milioni 500.

Kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam,watakubaliana na mimi kwamba zile sifa zilizokuwa zinavuma juu ya Mzee huyo akipewa kama Rais wa Jiji au Baba Makamba ndio zilianza kukoma baada ya kushindwa kuchukuwa hatua, kuna habari kuwa yale majina Mzee Makamba aliyakabizi wa Ikulu ya Utawala wa awamu ya tatu wa Benjamin Mkapa naye Majina yaliteketea wakati Ikulu ilipoungua kwa Mazingira ya kutatanisha kama sio kweli mbona hadi leo hatujaambiwa chanzo cha Ikulu kuungua Moto?


Namaliza kwa kukushukuru kujitolea kusema ukweli ingawa hadileo hakuna aliyetumia ushahidi wako kuwakamata wahusika lakini pia nakupa Pole kujitia kitanzi pasipo huruma kisha nakushauri kuwa ukitaka kupambana na Mafisadi kwa kusema ukweli ujiandae kusimama wala usikimbie tunajuwa wanasiasa hamkawiii kusema ulinunukuu vibaya.

mobinsons@yahoo.com 0753399 579

I

BINADAMU AMEJIANGAMIZA MWENYEWE

Sunday, March 11, 2007

MOBIN SARYA