Sunday, January 16, 2011

Zitto Ataka wazee wa Kigoma ‘kuwatia uchizi CCM.


Zitto sasa ataka ‘ndumba’ zitumike

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

MBUNGE machachari kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo Jimbo la Kigoma Kaskazini, Mhe. Zitto Zuberi Kabwe,katika hali ambayo haikutarajiwa na watanzania wengi,amewataka wazee wa Kigoma Ujiji warudishe zana zao ushirikina ili kuwaangamiza maadui zao.
Zitto aliyasema hayo hivi karibuni Mkoani humo kwa kuwashangaa wazee wa maeneo hayo kwa nini hawarushi zana zao kama zamani, kitendo ambacho kilichoupandisha chati Mkoa huo hali iliyosababisha jamii nyingine za Ki-tanzania kuhofia na kuogopa kwenda kuishi mkoani hapo.
“Zamani wazee wangu mlikuwa mkifanya vitu vikali hasa mkiona kijana wenu anaonewa au kudhulumiwa, lakini siku hizi mmepoa kweli”, alisema Zitto.
Aidha mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kupitia tiketi ya Chama cha cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliwaeleza wazee wa Kigoma Ujiji baada ya diwani wao kutoka Kata ya Vijiji kupata uchizi kitendo kilichosababisha ashindwe kuapishwa katika Baraza la kwanza la madiwani ambalo liliapishwa Desemba 20, Mwaka 2010.
Kitendo hicho alichodai kilichofanywa na wabaya wao dhidi ya diwani wao wa viti maalum wa Halmashauri ya Wilaya Vijijini ,kulichangiwa na sehemu kubwa ya Majimbo ya Mkoa wa Kigoma kunyakuliwa na vyama vya upinzani hali inayosababisha maadui zao kutumia ‘ndumba’ ili kudhoofisha ngome ya wapinzani.
“Nashukuru na wao CCM wanaye chizi, sijui mzee gani kakasirika na kumpa ugonjwa huo lakini ningeomba muwape madiwani wengine wawili uchizi ili wawe watatu”, alisema Mh, Zitto .
Alimaliza kwa kusema kuwa chama cha CCM kimekuwa na hulka ya kuwapunguza kasi viongozi wa Chadema kwa kuwapa chochote ili wakisaliti na kufuata matakwa yao,alidai kuwa diwani wa kata ya Katubuka alitaka kufanyiwa ‘kitu mbaya’ ila kwa mapenzi ya mola walishindwa kutimiza hila yao ya kumdhuru.
Kauli iyo iliyotolewa na Mbunge Zitto juu ya kuwataka wazee wa Mkoa wa Kigoma,imezuwa maswali mengi kutoka kwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa Mkoani humo,ambapo wengi walionekana kukerwa na kauli hiyo,waliyoieleza kuwa haikupaswa kutolewa na mtu kama Zitto Kabwe.
Wananchi hao waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti,wamesema kuwa Zitto,kijana msomi aliyerejesha matumaini makubwa kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma,ameonyesha kuwa bado ana safari ndefu kufikia kuwa mwanasiasa atakayeheshimika zaidi.
Wananchi hao,wameaambia mtandao wa www.mobinday.blogspot.com kuwa mtazamo huo mbaya wa Zitto,unaashiria kwamba hata yeye amekuwa akiamini mno ‘ndumba’,hali inayoshushia heshima yake katika jamii ya watanzania.
“Sikuweza kuamini kauli kama ile kutolewa na mtu mkubwa,tena aliyejijengea heshima kubwa sio hapa nchini tu,bali hata nje ya nchi,kuzungumzia masuala ya ‘ndumba’ katika karne hii ya 21 ya sayansi na teknolojia,tena msomi wa kiwango cha Zitto,kwa hakika imenisikitisha sana’’ alieleza mmoja wa wananchi waliojitokeza kuchangia hoja hiyo.
Zitto Kabwe,anatajwa kuwa ni miongoni mwa wanasiasa vijana waliotoa mchango mkubwa katika kuishinikiza serikali kupitia upya mikataba ya madini,ambayo ilikuwa ikiwanufaisha zaidi wawekezaji,na kuwaacha watanzania wakiendelea kudidimia katika rindi la umasikini.

Labels: