NILIWAHI kuandika jinsi ambavyo Jeshi la Polisi linavyochangia kuanguka upesi kwa dola inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), nilieleza jinsi matusi na lawama za wananchi dhidi ya Polisi zinavyoiathiri CCM.
Nilieleza kwa makini jinsi taasisi mbalimbali za Serikali zinavyochangia kuanguka kwa haraka Chama cha Mapinduzi, kwasababu Mwenyekiti wake ndiye Mkuu wa Serikali iliyopo madarakani.
http://www.bongoradio.com/news_image/133_killingofdaudi.jpg

Lakini leo kutokana na kifo cha Mwanahabari wa Kituo cha Televisheni ya Chanel 10, Daud Mwangosi aliyeuwawa kikatili na ‘jeshi la Polisi’ naenda mbali zaidi kwa kusema Polisi wanachangia,watachangia Rais Jakaya Kikwete kuikosa tuzo ya utawala bora inayojulikana kama MO IBRAHIM.
Tuzo hiyo iliyoasisiwa na tajiri raia wa Sudan, hutolewa kwa viongozi wastaafu wa Afrika waliosimamia utawala bora enzi wakiwa madarakani na kuna wakati taasisi hiyo imeshindwa kumpata kiongozi wa kumpa baada y viongozi wastaafu kukosa sifa akiwemo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.]
Hali hiyo huenda ikamkumba Rais Kikwete akabaki kuwa msindikizaji baada ya kushindwa kusimamia utawala bora unaosababisha raia wake kuwawa kila kukicha na viongozi wa Serikali hususani askari wa Polisi.
Tukio kama hili la Mwandishi wa Chanel 10 kuwawa hadharani tena kikatili na askari wa Jeshi la Polisi sio tu kwamba limeifedhehesha Serikali, bali hata taswira ya nchi na utawala wa rais Kikwete umechafuka nje ya mipaka yetu.
Kilichochafua Serikali ni jinsi inavyoonekana kwenye picha mwandishi asiye na silaha akiwa na kamera yake huku akizungukwa na mapolisi wenye nguvu na kumshughulikia kama vile wanamdhibiti mhalifu sugu aliyekuwa anatafutwa siku nyingi.
Katikati ya purukushani hiyo askari aliyefunzwa mafunzo ya kuzima vurugu na kudhibiti vibaka anamwelekezea mtutu wa bunduki kisha anamumiminia mabomu mwanahabari asiyekuwa na kosa lolote ambaye amri ya kuwataka wafuasi wa CHADEMA waondoke katika eneo la tukio.
Tunachojiuliza kama mwanahabari asiyekuwa na silaha anauwawa mbele ya Mkuu wa Kituo cha Polisi na RPC, Usalama wa waandishi wa habari wanapokuwa kwenye shughuli zao zinazohusiana na machafuko ukoje?.
Leo mwandishi wa habari anapochinjwa kama kuku mchana kweupe mbele ya viongozi wa Polisi na hadhara, je ni wananchi wa ngapi wameuwawa kikatili na kusingiziwa kuwa walikuwa wanafanya makosa ambayo hawajafanya?.
Wakati tukijiuliza maswali hayo,bila shaka nchi zingine zitakuwa zinatutazama kama nchi ya vichaa, kwa kuwapatia askari silaha za moto bila kuwafanyia uchunguzi uwezo wao wa kiakili kama wanaafya njema.
Askari wetu walipofikia ni mahali ambapo sasa kabla hawajapewa silaha na kutakiwa kwenda mbele ya hadhara wapimwe kwanza kiwango cha alkoho au nicotini kilichopo mwilini mwao kabla ya kuruhusiwa kwenye mazozezi ya kutuliza ghasia, vingenevyo ipo siku watakapomaliza kutuua wataanza kuuwana.
Hiyo inatokana na madai kuwa baadhi ya askari wamekuwa na kasumba ya kutumia sigara kubwa maarufu kama bangi wanapojiandaa kwenda kwenye kazi zao na madai kama hayo yamewahi kutolewa na mkulima mmoja wilayani Tarime aliyesema kuwa japo Polisi wanasema bangi ni haramu, lakini wateja wetu wakubwa ni wao.
Madai hayo yanaungwa mkono na picha zilizopigwa eneo la tukio wakati askari wakimnyanyasa kwa kumsulubu Mwangosi kabla ya kumuua zinamuonyesha Marehemu akiwa amemkumbatia Mkuu wa Polisi OCD Wilaya ya Iringa, lakini hapo pote askari wanalipua mabomu.
Huu ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa askari kulipua mabomu mbele ya wakubwa zake na kusababisha maafa makubwa kama hayo yaliyosababisha bosi wake kuvunjika mguu kwasababu ya askari ambaye pengine kabla ya kukabidhiwa silaha alitumia sigara kubwa.
Tukio la kuuwawa kwa mwanahabari huyo limekuja wiki mbili baada ya tukio lingine kama hilo kutokea mkoani Morogoro na safari hiyo aliuwawa muuza magazeti ambaye wala hakuwa sehemu ya walengwa.
Mauaji kama hayo na mengine ambayo yalitokea mkoani Arusha, Mara na Mwanza yanazidi kuchagiza kuondoka madarakani kwa Chama cha Mapinduzi kwasababu lawama zote zinawaelekea viongozi wa CCM, kwamba ndio wameshindwa kusimamia dola inayoheshimu utawala bora.
Wadau wa habari tunamuomba rais Kikwete asimame atazame wale wanaovunja utawala bora wakidhani kwamba wanalinda utawala wake, kumbe wanamwangamiza na chama chake ili akosema sehemu ya kupumzika atakapostaafu.
Ifikie mahali sasa Rais atoe tamko kueleza umma hisia zake kwa kifo cha mwandishi huyo wa habari ambaye alikuwa anatumika kuchukua matukio wakati akifanya ziara mkoani Iringa, lakini leo amefariki Rais ameshindwa kutuma hata rambirambi kama ambavyo amekuwa akifanya kwa misiba mingine.
Rais Kikwete kama anania ya kusifiwa kwa mazuri baada ya kustaafu ni wakati sasa kusimama na kukemea vitendo hatarishi vya utawala bora vingenevyo siku moja mauaji haya yanaweza kumletea machafuko akashindwa kukaa hata huko Ikulu.
Wadau wa habari tunajiuliza kama leo mwanahabari anauwawa kinyama tena hadharani je kesho ni nani atauwawa katika mazingira kama hayo?,usalama wa viongozi wa vyama vya siasa wanaondeleza harakati za mageuzi uko wapi?, Je, wandishi wa habari bado tuna ari ya kuendelea kushirikiana na Polisi kufanyakazi kama awali tulivyokuwa tunafanya? .
Hayo ni maswali ya kujiuliza wakati huu wa maombolezo ya msiba yaliyoikuta Tasnia ya habari huku tukimuonea huruma rais Kikwete jinsi alivyozidi kuikimbia tuzo ya utawala bora inayotolewa na Mo Ibrahim!.
Binafsi nasema endapo chama tawala hakitakuwa makini na matukio yanayofanywa na Jeshi la Polisi, basi kitahukumiwa kwa gharama yoyote ingawa sikitakii mabaya hayo ambayo ni bomu ambalo linatengenezwa na chombo chake chenyewe.
Hili ni bomu linalotengenezwa na Jeshi la Polisi dhidi ya CCM, lakini pia Serikali lazima iwaandae askari wake kiakili namna ya kukabiliana na akili za wanasiasa, sio lazima kutumia nguvu nyingi sana bali wapewa ama wajengewe uwezo wa kufikiri zaidi ya wanasiasa.
Je,askari wetu wamefika mwisho wa kufikiri zaidi ya kuuwa raia?,kama hawajafikia mwisho wa kufikiri wanafikiriwa na nani kwa niaba ya nani?,kwa ujira upi zaidi ya kodi za wale wanaowafyatulia risasi.
Kama Polisi wanaua walipa kodi nani atawalipa mishahara?. Je,polisi wetu ndivyo wanavyotumwa baada ya mafunzo?. Je, mauaji ya mwandishi ama mauji yaliyotokea huko Morogoro na mengine yanayohusishwa na siasa nani alaumiwe?. Je,vilaumiwe vyama vya siasa ama Jeshi la Polisi?.
Mwandishi wa makala hii ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wasio na Ajira ya Kudumu (TCJ) na anapatikana kwa simu: 0753 399 579