Wednesday, February 22, 2012

Wanaoikimbia CUF ni makanjanja wa siasa

Na Mobini Sarya

TANGU kuibuka kwa mtafaruku ndani ya chama cha wananchi CUF baadaye kutimliwa uanachama kwa mbunge wa Jimbo la Wawi (Pemba)Hamad Rashid na wafuasi wake mengi yametokea.


katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF, Maalim Seif Hamad

Kinachoonekana hivi sasa kuendelea katika chama hicho ni hujuma ya wazi ambazo kama viongozi wa CUF wasipo kuwa makini Demokrasia inaweza kupata pigo zaidi.
Kwa wale tunaounga mkono ustawi wa Demokrasia hapa nchini hatupendi kuyaona yanatokea haya yanayoendelea sasa , huku tukihoji wahusika kuwa leo CUF ikiporomoka ni kwa faida ya nani?
Ninani ananufaika na mgogoro wa CUF?kuanguka au kusimama kwa chama hiki mhimu kwa mstakabali wa siasa kuna maana gani katika mstakabali wa siasa za taifa letu?
Maswali hayo yanatokana na ukweli kuwa hali ya mwenendo wa siasa ndani ya CUF ilivyo hivi sasa siyo ya kuridhisha jambo linalotukatisha tama na kututia hofu wale tuliokuwa na mategemeo ya kuona siku moja chama cha mapinduzi (CCM)kinakabidhi dola kwa amani bila risasi.
Lakini sasa hali inavyokwenda CUF mbapo kumeibuka makundi ya wananchama mbali mbali wanaotangaza kung’atuka kwenye chama hicho kunatoa frusa kwa CCM iendelee kutanua kwa miongo kadhaa jambo ambalo ni hatari katika jamii inayohitaji mabadiliko.
Hali hiyo ndio inatufanya baadhi yetu tuamini kuwa inawezekana mgogoro ulioikumba CUF ukawa ni kansa iliyopandikizwa kutoka nje ili kukifuruga chama hicho kwa kuwarubuni wanachama makanjanja waliokuwa kwenye msafara wa Demokrasia.
Ukiwasikiliza kauli zao wale wanaojitoa CUF utabaini kuwa kama ni utashi wao basi hawakuwa na sababu ya kukimbia chama chao cha CUF zaidi ya hujuma.
Baadhi yao wanakimbia chama hicho wakidai kuwa, Katibu mkuu wa Chama hicho Maalim Seif anakiharibu hawasemi ananavyokiharibu zaidi ya kuishia kumpaka matope.
Kwa wale tunaofatilia hali ya mambo ndani ya chama hicho tunaweza kusema kuwa wanasiasa wengi wanaokimbia chama hicho ni makanjanja wa Siasa wanaofuata upepo wa siasa na Posho.
Wameamua kukimbia wakagange njaa walipoahidiwa mema,inawezekana wengine wamefikia hatua ya kuahidiwa kuwa watapewa chochote kama wataamua kuondoka CUF kwa kutangaza kwenye vyombo vya habari.
Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa haiwezikani wanachama zaidi ya watatu wanaoishi maeneo ya mitaa tofauti waamke wote na kutangaza kuwa wanahama CUF bila kuwepo mpango wa kuratibu zoezi hilo.
Leo makundi ya wanachama wamekuwa wakisikika maeneo mbalimbali wakidai kukihama chama hicho, kwa madai kuwa hawana imani na katibu mkuu wao.
Hawana imani na Katibu mkuu?miaka yote wamekaa naye?amewawezesha kuunda Serikali ya mseto baada ya kuibana vilivyo CCM,waje waseme Maalim Seif anaua chama! Kwa vipi hawatuelezi.
Madai ya Katibu mkuu kuua Chama yameanza kutolewa baada ya kuendesha kikao kilichomg’oa uanachama mjumbe wa Baraza kuu,Hamad Rashid na wafuasi wake ambao sasa inawezekana ndio wanatumiwa kama mamluki kuiangamiza Demokrasia.
Tunapaswa kutambua kuwa katika mfumo wa siasa ya vyama vingi kuna makanjanja wa Siasa ambao kazi yao ni kuhama wanatafuta mlo japo wa siku moja lakini ukiwachunguza kiukweli sio wanasiasa makini.
Wanaendelea kuzunguka huku na kule wakifuatilia uvumi wa upepo kisiasa lakini mwisho wa siku hupoteza hata ule mtaji mdogo wa siasa waliokuwa nao, kama ambavyo tumepata kuwaona wanasiasa wengine waliotangulia.
Kwa uchache hapa nchini walikuwepo nguli wa siasa kama Hiza Tambwe aliyekuwa anatamba katika Manisapaa ya Temeke,akiwa CUF lakini tangu alipofuata upepo unapovuma kuelekea ameanguka shimoni.
Bado wengine wanachechemea kama Agoustine Lyotonga Mrema aliyefikia hatua ya kuomba japo awe Rais kwa dakika tano ,John Momose Cheyo aliyewahidi watanzania kuwajaza mapesa lakini baada ya kuingia kwenye siasa za migogoro walioumia ni watanzania kwa kupoteza demokrasia.
Bila kusahau kuna majina mengine yanaelekea kufutika kabisa kama sio kusahaulika ambao ni Jidula Mabambasi,Wilfred Lwakatare na wengine kibao ambao waliteteleka kidogo wakazolewa na siasa za upepo.
Kwa hiyo napenda kumashauri Mbunge wa Wawi Hamad Rashid asijaribu kuivuruga Cuf akidhani kuwa kama ataondoka na kuanzisha chama kinaweza kupata nguvu zaidi ya chama chake cha awali.
Kama anabisha awaulize wananchama wa Sauti ya UMMA waliokimbia CHADEMA kama wamefanikiwa hata kumpata Diwani mmoja tangu wajiengue chadema na kuanzisha chama kipya.
Pia waulize wasisi wa Chama cha Jamii (CCJ) ambao wamekibadilisha jina na sasa kinajulikana kama CCK ile nguvu na msukumo waliyokuwa nayo kipindi kile sasa iko wapi tangu kimesajiliwa mbona wameshindwa hata kusimamisha wagombea katika majimbo madogo kama Uzini na Arumeru.
Ni ukweli usiopingika kwamba CUF ikiyumba na serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar itayumba jambo litakalorudisha Demokrasia nyuma na kukifanya CCM kipumue kuelekea uchaguzi wa Mwaka 2015,je tukifikia hapo Hamad Rashid atakuwa amevuna nini?
Hivi anajua kuwa kabla chama cha CUF hakijapata mizizi Zanzibar ndugu zake wapemba walikuwa wanabaguliwa katika masuala ya maendeleo, lakini leo wanapata umeme, maji na uwanja wa ndege umeanza kujengwa kule kwao.
Hivi vitu havitakuwepo kama CUF itazorota na kushindwa kuisimamia kwa makini serikali ya mapinduzi ,itakapofikia hapo wafuasi wa hamadi Rashid wataficha wapi uso wao itakapoelezwa kwenye historia kuwa ukanja nja wao ndio ulichangia kuhujumu Demokrasia iliyokuwa imepatikana.
Aidha kwa upande wa viongozi wa CUF nao wanakesi ya kujibu kama watakaa kimya na kuacha chama hicho kiendelee kuzorota bila kuchukua jitihada zozote za kuanza kuzunguka kwa wanachama na kuwaleza kinachoendelea ndani ya chama chao.
Ni wakati muafaka sasa kufufua oparesheni nyuki na kuanza kushambulia katika mikoa mbalimbali kwa kurudisha imani ya wananchama wao kuliko ilivyo sasa ambapo wanachama wanashindwa kuamini kinachotokea kwenye vyombo vya habari.

Labels: