TUPO NCHI ZA WATU
Innocent Nganyagwa
KARIBU msomaji wa safu yetu ya mambo ya kijadi ya Kiafrika, inayokujia kila siku ya Jumamosi, tunapokutana kwenye ukurasa huu wa gazeti lako ulipendalo la Tanzania Daima, Sauti ya Watu.
Kupitia safu hii tunapata fursa ya kuelimishana juu ya mambo mbalimbali ya utamaduni na jadi zetu zinazotutambulisha na kuakisi Uafrika wetu halisi.
Leo kwa mara ya tatu tunawatembelea tena ndugu zetu Wakurya, kabila kutoka upande wa kaskazini mwa nchi yetu katika Mkoa wa Mara.
Kwa kawaida huwa tunatembelea kabila moja kwa wiki mbili tu, lakini kutokana na asili yao walikotokea watu wa kabila hili, ambako ni mbali sana kwa kweli, imetupasa tuanzie nyuma zaidi na kuja nao taratibu mpaka walipofika eneo walilopo hivi sasa ili uweze kuwaelewa vyema ndugu msomaji.
Hiyo itakupa picha halisi ya mambo yao kama ule ubabe wao wa kupigana pigana, japo mara nyingi hupigana zaidi kati yao wenyewe kuliko kupigana na makabila mengine.
Wakurya kama tulivyoona wiki iliyopita, wanatokana na moja ya jamii za mashariki ya kati zilizovuka na kuingia Afrika kaskazini na huko kuchanganyika na Waafrika weusi.
Kutoka kule mashariki ya kati ni maeneo ya Israel na Syria, utakumbuka niligusia kidogo wiki iliyopita juu ya Wanyabhasi, kundi la Wakurya wenye utukufu wa Wayahudi weusi na linaloheshimiwa sana na Wakurya wengine.
Sasa basi, kutoka Afrika kaskazini wakamegeka na kuanza kuja upande wa kusini, nadhani bado unakumbuka tulivyosema kuwa hawa jamaa walikuwa na tabia ya kuweka makazi katika eneo moja na likishachakaa huhama na kwenda kwingine, tabia iliyowapatia sifa ya jina lao la Ba-kurya.
Kusafiri huko kwa kuhamahama hatimaye kuliwafikisha katika bonde la Mto Nile walikoweka kituo cha muda mrefu sana, yapo makabila mengine pia yaliyoweka kituo katika bonde hilo, haya yote kwa jina la kiujumla huitwa ‘Nilotes’, yaani wakazi wa asili ya pembezoni mwa Mto Nile.
Kama unaifahamu vyema jiografia, basi kuwepo kwao hao Wakurya kwenye bonde hilo kumesababisha wawepo pia katika nchi zinazopitiwa na mto na bonde hilo, ndio maana katika sehemu ya kwanza nilikutaarifu kuwa wanapatikana pia huko Sudan, Uganda na Kenya.
Tena huko Kenya wana sehemu yao kabisa inayoitwa Kurya na ni huko ndiko walikopata sifa ya ukorofi kwa mkong’oto waliowapa Wakisii. Kumbuka tulisema kuwa hawa Wakurya walijifunza kupigana na kutengeneza silaha kutokana na kukumbana na mikasa mingi ya mapigano pale jamii zao za awali zilipokuwa zinakuja huku kusini kutokea kaskazini.
Mpaka hapo hutashangaa kujua kwanini kuna wapiganaji wengi wa Kikurya katika jeshi letu, maana hawa jamaa ni mashujaa wasio na woga na wanaofahamu sana kupigana, hiyo ni moja kati ya sifa za jamii za watu wa mashariki ya kati.
Natumaini kuhusu walikotoka mpaka jinsi walivyofika hapa nchini tumeelewana, sasa tujikite zaidi katika mambo yao ya kijadi katika eneo walilopo hivi sasa.
Kwanza naomba nifanye masahihisho kidogo kutokana na makosa ya uchapaji ya neno ‘wasamba’ ambalo lilitokea kama ‘wasambi’ katika sehemu yetu ya pili wiki iliyopita.
Neno lililodhamiriwa ni ‘wasamba’ lenye maana ya wengi linaloonyesha mjumuiko wa vijana wengi wanaotoka jandoni baada ya kumaliza kipindi cha kukaa huko tangu pale walipotahiriwa.
Kwa kawaida, kijana akishatahiriwa huingia katika kipindi anachoitwa ‘omosamba’ na huendelea hivyo hadi atakapofanyiwa sherehe ya kumaliza kipindi hicho, ambacho huchukua takriban mwezi mmoja hadi miwili hivi.
Sherehe huandaliwa kwa ajili ya ‘okooroka’, yaani anapotoka katika kipindi cha ‘omosamba’ na kuingia katika rika analochukuliwa kuwa sasa ni mtu mzima.
Hapo ndipo sasa anakuwa huru kuanza kujihusisha na hatua ya kuoa au kuolewa. Tukiendelea kuzama kwa kina zaidi juu ya ndugu zetu hawa, utakumbuka kuwa hapo awali katika sehemu zilizopita nilikufahamisha juu ya mambo yao ya imani za asili.
Tuliona kuwa jua lina nafasi kubwa na ya muhimu zaidi katika imani yao, kumbuka pia tulishawahi kuyatembelea makabila mengine mawili yanayotilia maanani umuhimu mkubwa wa jua kiimani, hao ni Wazanaki na Wachagga. Nitakufafanulia ni kwanini jua lilipewa umuhimu huo mkubwa kiimani.
Ufafanuzi wa kwanza ni wa tabia za kiujumla za makabila yanayotokana na mbari ‘race’ moja au kama jamii zao zilikutana na kukaa eneo moja kwa muda mrefu sana kiasi cha kuchanganya asili na baadhi ya mambo yao ya kijadi.
Yale makabila mengine niliyoyataja hapo juu, nayo pia jamii zake za mwanzo zilishawahi kuwa katika eneo la bonde la Mto Nile. Hayo na makabila mengineyo, mengi kati yao yanaamini katika jua.
Ila kwa Wakurya, wana sababu za ziada za kuamini katika nguvu ya jua ambazo zinatokana na huko walikotokea hapo awali, mashariki ya kati. Mfano mmojawapo ni kwenye imani za Kiyahudi, natumaini bado unakumbuka mambo ya lile kundi la Wakurya la Wanyabhasi ‘wayahudi weusi’- kwenye baadhi ya masimulizi ya maandiko ya Agano la Kale, kuna kisa cha mke aliyedai kupata ujauzito wa mume wake aliyefariki muda mrefu uliopita.
Aliupata ujauzito huo kupitia kwenye nuru ya jua kutoka kwa huyo marehemu mumewe, hicho ni kisa cha mtoto Tamuz, aliyezaliwa kwa uwezo wa jua na mama yake Semiramis.
Tukirudi hapa walipo sasa, jua kwao lilifananishwa na nuru na kuaminika kuwa lina nguvu ya Mungu kutokana na uwezo wake. Imani hii waliithamini sana, hasa kutokana na kuwa, katika kabila lao watu waliochukuliwa kama manabii kutokana na uwezo wao wa kuona maono ya mambo yatakayotukia hapo baadaye, mara nyingi walidai kutokewa na nuru ya mwanga wakati wa kupata ufunuo wa tafsiri za maono hayo hata kama ni usiku wa manane.
Nuru hiyo ikahusishwa na jua lenye nuru kuu, hivyo kusababisha kuamini kuwa nguvu ya Mungu kuwafahamisha kuhusu mambo mbalimbali hupitia kwenye jua, kwa maana hiyo basi, anaishi kwenye hilo jua.
Msomaji, si hawa Ba-Kurya tu wanaoamini kwenye mambo hayo ya jua, hata baadhi ya mataifa yameweka alama yake kwenye bendera zake katika ile hali ya kulipa utukufu kutokana na umuhimu wake, japo hawana mtazamo wa pamoja kiimani katika kulielekea hilo jua.
Nikulete kwenye jambo lingine la mambo hayo ya alama linalofanana na mambo hayo ya jua ndani ya kabila hilo. Wakurya ni wala nyama, lakini katika ulaji wao huo wa nyama, wana miiko ya kutokuwala baadhi ya wanyama kutokana na sababu mbalimbali.
Kati ya wanyama wasiowala, ni pamoja na wale wanaokula binadamu na wale ambao si kawaida kuliwa kama vile fisi. Lakini pia hawali wanyama kama tembo na nguruwe. Nitatoa ufafanuzi wa jambo hilo unaohusu maeneo yao wanayoishi.
Katika maeneo yao, kuna tarafa zipatazo nane, nne zikiwa katika maeneo yanayokaliwa zaidi na Wajaluo na nne nyingine zikiwa katika maeneo wanayokaa wao.
Tatu kati ya tarafa nne zilizo upande wao, zinaitwa ‘Inchughu’, yaani tembo kwa lugha yao, halikadhalika zile nyingine mbili zikiitwa ‘Ingwe’, yaani chui na ‘Inchaghe’ ambaye ni pundamilia. Sababu ya tarafa hizo kuwa na majina hayo ni kwamba, kuna kuhusika kihistoria juu ya wanyama hao kama nembo ya kiimani kijamii kwa wale walioishi huko hapo awali.
Sifa za kiimani za kuitwa majina hayo hata hivyo zilitokana na mafungu ya kijamii ya watu wa kabila hilo, mathalan wale Wanyabhasi hupatikana sana huko Inchaghe. Imani hizo za kialama zilisababisha heshima fulani juu ya wanyama hao waliogeuka nembo muhimu, hivyo kutoliwa.
Ila kuhusu nguruwe, ni kutokana na imani za jamii zao za awali, tangu wakati wa u-mashariki ya kati. Kwahiyo, hawa ni watu wa imani na wanaziheshimu sana, mathalan walitenga siku maalum ya kuabudu kama walivyokuwa huko mashariki ya kati, hilo hasa lilifanywa zaidi na wale ‘Wayahudi weusi’ - Wanyabhasi.
Kwa kumalizia ng’we ya leo, nikufahamishe kwamba, ukichunguza kwa makini utagundua kuwa jamii tangu awali zilijenga tabia ya kuwatumia wanyama kama nembo au ishara za kujivunia nazo kutokana na mambo yao mbalimbali.
Mambo hayo yalivuka na kuja kuingia katika alama muhimu za mataifa miaka ya baadaye baada ya makundi ya makabila kukaa pamoja na kujitambua kama taifa moja.
Kwa msingi huo, utakuta kama si kwenye bendera, basi hata kwenye nembo za kitaifa kuna utukufu huo wa wanyama. Baadhi ya mifano ya alama za wanyama kitaifa ni: Kenya (Simba), Tanzania (Twiga), Uganda (Kolongo), Nigeria (Mwewe), Senegal (Simba) na hata Marekani (Tai).
Wiki ijayo tutapiga hodi ya mwisho na kumalizana na ndugu zetu hawa kabla ya kuanza kulitafuta kabila lingine la kulitembelea na kufahamu mambo yake. Alamsik!
Simu: +255 752 227 594.
