Friday, February 25, 2011

SERIKALI yajitenga na machafuko Libya


SERIKALI imesema kuwa haiwezi kutoa kauli yoyote kuhusiana na machafuko yanayoendelea nchini libya kwasababu kauli hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa watanzania wanaokaa huko.

Akizungumza leo Dar salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe amesema kuwa ikiwa serikali itatoa maoni yoyote kuhusiana na machafuko hayo walibya wanaweza kukasirishwa na kauli hiyo wakawashambuliwa watanzania.

Waziri Membe amesemba kuwa Tanzania imejiandaa kuwarejesha nyumbani watanzania wote wanaokaa Libya kama wataona maisha yao yako hatarini na tayari imeagiza wajiorozeshe.

Akizungumzia wanafunzi wanaosoma libya amesema kuwa tayari wamewakusanya 22 ambao wanatarajiwa kuwasili leo kupitia ubalozi wa Kenya nchini Libya ambao umetuma ndege kwa ajili ya kuwahamisha wakenya.

Amesema kuwa maofisa wa ubalozi wa Tanzania, mjini Cairo Misri wamewasiliana na ubalozi wa Kenya Tripoli ,kwa kuwa Tanzania haina ubalozi Libya, ili kuhakisha wanafunzi hao wanarejea nchini leo jioni wakiwemo watanzania sita.

Membe amesema kuwa nchi ambazo zilijaribu kueleza machafuko yaliyokuwa yanatokea Misri zilipata hasara kwa wananchi wake kushambuliwa pamoja na makampuni yao kuporwa, huku Tanzania ikirejesha wanafunzi 50 nyumbani ambao wanatarajiwa kurejea nchini humo baada hali kutulia.

Aidha katika hatua nyingine waziri huyo amesema kuwa viongozi wa nchini watano wanaounda kamati ya usuluhishi katika mgogoro wa Ivory Cost inatarajiwa kukutana mjini Abjan kwa ajili ya kutoa tamko rasmi ambalo litawakilisha msimamo wa baraza la usalama la Afrika.
Membe amesema kuwa hatua inatokana na kamati hiyo inayomjumisha Rais Jakaya Kikwete na Jacob Zuma wa Afrika kusini kukutana Feburuary 21 Mjini Mauritania, ambapo Rais wake ni mwenyeki wa kamati hiyo kasha kwenda Ivory Cost kukutana na viongozi wanaohusika na mgogoro wa kugombea madaraka.

Wednesday, February 23, 2011

HUYO NDIYE MMILIKI WADOWANS


HATIMAYE SASA WAHARIRI WATAPUMUA BAADA YA PICHA HII KUPATIKA
MMILIKI aliye na hisa nyingi katika kampuni za Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd, Sulaiman Al Adawi, amehitimisha ziara yake nchini jana baada ya kukutana na Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal, ofisini kwake jana.
Kabla ya kukutana na Bilal ambaye ndiye aliyekuwa akikaimu nafasi ya urais kutokana na Rais Jakaya Kikwete kuwa nje ya nchi kikazi, mfanyabiashara huyo (pichani) alikutana na uongozi wa juu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO).
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumatano imezinasa kutoka vyanzo vya kuaminika serikalini zinaeleza kuwa wakati wote akiwa katika mazungumza na Dk. Bilal na hata baada ya kumaliza mkutano wao, Adawi alikataa katakata kupigwa picha.
Chanzo cha kuaminika cha habari hizo kilieleza kwamba katika mazungumzo yao Dk. Bilal na Adawi walijadili masuala yaliyokuwa yakielezea kuhusu uwekezaji na matatizo yale yanayoikabili kampuni yake ya Dowans.
Habari zaidi zinaeleza kuwa siku mbili kabla ya kuzungumza na Dk. Bilal, bilionea huyo wa Dowans ambaye taarifa za kuwapo kwake nchini zimeibua maneno mengi, alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando.
Ilielezwa kwamba katika kikao chake na Mhando, aliwasilisha barua ambayo ilionyesha utayari wa kampuni yake kujadiliana na Tanesco na kupunguza kiwango cha fidia cha dola za Marekani milioni 64 (sawa na shilingi bilioni 94) ambacho shirika hilo la umma linapaswa kuilipa Dowans kutokana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICC).
Habari za uhakika zinaeleza kwamba Dowans walikuwa tayari kusamehe zaidi ya dola za Marekani milioni 40 kwa Tanesco na wakati huo huo kukaa chini na shirika hilo kwa ajili ya kuingia mkataba mwingine na shirika hilo ambao wanadai utakuwa nafuu zaidi kuliko ilivyo kwa wazalishaji wengine wanaoliuzia umeme shirika hilo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Tanesco na ndani ya Dowans zinaeleza kwamba hadi kufikia jana mchana, mkataba huo ulikuwa haujatiwa saini na hivyo kusababisha mmiliki wa kampuni hiyo kuondoka nchini jana jioni na kuliacha suala hilo kwa wasaidizi wake.