Wednesday, February 23, 2011

HUYO NDIYE MMILIKI WADOWANS


HATIMAYE SASA WAHARIRI WATAPUMUA BAADA YA PICHA HII KUPATIKA
MMILIKI aliye na hisa nyingi katika kampuni za Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd, Sulaiman Al Adawi, amehitimisha ziara yake nchini jana baada ya kukutana na Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal, ofisini kwake jana.
Kabla ya kukutana na Bilal ambaye ndiye aliyekuwa akikaimu nafasi ya urais kutokana na Rais Jakaya Kikwete kuwa nje ya nchi kikazi, mfanyabiashara huyo (pichani) alikutana na uongozi wa juu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO).
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumatano imezinasa kutoka vyanzo vya kuaminika serikalini zinaeleza kuwa wakati wote akiwa katika mazungumza na Dk. Bilal na hata baada ya kumaliza mkutano wao, Adawi alikataa katakata kupigwa picha.
Chanzo cha kuaminika cha habari hizo kilieleza kwamba katika mazungumzo yao Dk. Bilal na Adawi walijadili masuala yaliyokuwa yakielezea kuhusu uwekezaji na matatizo yale yanayoikabili kampuni yake ya Dowans.
Habari zaidi zinaeleza kuwa siku mbili kabla ya kuzungumza na Dk. Bilal, bilionea huyo wa Dowans ambaye taarifa za kuwapo kwake nchini zimeibua maneno mengi, alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando.
Ilielezwa kwamba katika kikao chake na Mhando, aliwasilisha barua ambayo ilionyesha utayari wa kampuni yake kujadiliana na Tanesco na kupunguza kiwango cha fidia cha dola za Marekani milioni 64 (sawa na shilingi bilioni 94) ambacho shirika hilo la umma linapaswa kuilipa Dowans kutokana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICC).
Habari za uhakika zinaeleza kwamba Dowans walikuwa tayari kusamehe zaidi ya dola za Marekani milioni 40 kwa Tanesco na wakati huo huo kukaa chini na shirika hilo kwa ajili ya kuingia mkataba mwingine na shirika hilo ambao wanadai utakuwa nafuu zaidi kuliko ilivyo kwa wazalishaji wengine wanaoliuzia umeme shirika hilo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Tanesco na ndani ya Dowans zinaeleza kwamba hadi kufikia jana mchana, mkataba huo ulikuwa haujatiwa saini na hivyo kusababisha mmiliki wa kampuni hiyo kuondoka nchini jana jioni na kuliacha suala hilo kwa wasaidizi wake.

0 Comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA NDUGU

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home