Wednesday, November 7, 2007

MAISHA YETU

Elewa msongo wa mawazo

Na Lucy Ngowi

Si vibaya nikianza kumshukuru Mungu kwa kunifikisha siku na wakati kama huu. Naamini hata wewe msomaji wangu una kila sababu ya kumshukuru Muumba wetu, kwa kukumbushia tu, leo tunaendelea na mada yetu ambayo ilianza wiki iliyopita inayozungumzia msongo wa mawazo ambao humpata mtu kutokana na mambo mbali mbali anayokumbana nayo katika maisha. Tutaangalia maana, dalili, vitu vinavyosababisha, matokeo na jinsi ya kutatua hali hiyo, endelea.
WOTE tunakabiliana na changamoto na vikwazo mbalimbali, hata wakati mwingine tatizo linakuwa kubwa kukabiliana nalo. Inafikia mahali tunajihisi kuzidiwa, au kuwa chini ya mtutu wa bunduki, au kutokuwa na uhakika wa jinsi tutakavyotimiza mahitaji ambayo yako juu yetu, hapo huwa tunakuwa na msongo.
Iwapo utakuwa katika kiwango kidogo, msongo unaweza kuwa kitu kizuri. Msongo unaweza kukupa msukumo wa kile unachokihitaji, unaweza kukupa motisha wa kufanya vizuri zaidi na kuwa mtu mwenye malengo siku zote.
Msongo unaweza kukufanya uwe makini kwa mfano kama unasoma, unaweza kukufanya uwe makini na masomo wakati wa likizo badala ya kukaa ukiangalia Tv. Lakini mambo yanapokuwa magumu na mahitaji ya maisha yakazidi uwezo wako wa kuyatimiza, hapo ndipo msongo huwa tishio kwako kimwili na kihisia pia.
Wiki iliyopita tuliona baadhi ya sababu zinazosababisha msongo wa mawazo, leo tutaangalia sababu nyingine zaidi zinazochangia tatizo hilo.
Mojawapo ya sababu hizo ni pamoja na maisha yasiyo na uhakika ‘maisha kamari.’
Wataalamu wengi wanaamini kuwa kutokuwa na maisha ya uhakika ni moja ya sababu za msongo.
Wengi tumekuwa watumwa wa maisha ya kisasa tukitaka kuishi katika daraja ambalo si letu. “Wote tunataka kuwa maarufu, matajiri, washindi wa bahati nasibu,” anasem mwanasaikolojia Patrick Whiteside, mtunzi wa kitabu kijulikanacho kama ‘little Book of Bliss’.
Aina hii ya utamaduni unatuweka katika shinikizo. Watu wanajishurutisha ili waweze kuwa na mafanikio na pesa, wanataka kuwa na nyumba kubwa, televisheni kubwa na magari ya thamani kubwa, lakini wanasahau umuhimu wa kuwa wenzi wazuri katika familia zao,” anasema.
Mara nyingi, mtu anajikuta hana uchaguzi ila kuendelea na hali ya mawazo. Lakini ni muhimu ukathubutu kujaribu na kurudi nyuma huku ukifikiria juu ya uchaguzi ulioufanya awali. Kufikiria juu ya mabadiliko unayoweza kuyafanya kulingana na aina ya maisha unayoishi.
Kama hali ya mawazo inaendelea, inaweza kuleta matatizo makubwa katika kutekeleza majukumu ya kitaalamu kulingana na fani yako au maisha, au hata kuathiri afya yako.
Sababu nyingine ni matatizo ya kiuchumi. Kama mtu hana fedha za kukidhi mahitaji ya muhimu atajikuta katika hali mbaya ya kuwaza ambayo inaweza kumsababishia msongo.
Mtu huyo atajikuta katika lindi la mawazo , akijaribu kufikiri jinsi atakavyopata fedha kwa ajili ya kufanya biashara, au kusomesha mtoto au hata itakayomwezesha kuishi maisha mazuri.
Mwingine unaweza kukuta akiwaza juu ya nyumba na anataka kuishi katika nyumba ya hadhi fulani lakini hana uwezo wa kufanya hivyo, au pengine kuharakishwa kutoka katika nyumba katika kipindi ambacho alikuwa hajawa tayari kufanya hivyo, hayo pia yanaweza kuwa matatizo ambayo yanaweza kuleta msongo.
Sababu za msongo zina wigo mkubwa, wakati mwingine unaweza kukuta mtu anapata shinikizo kutoka kwa bosi wake, au hata ndugu anaoishi nao kama vile shemeji au wifi, au wakati mwingine kuachishwa kazi au kustaafu akiwa hajajiandaa.
Kwa wale wanaostaafu hupatwa na msongo pale ambapo hujikuta wakitakiwa kuachia nyadhifa zao wakati hawajajiandaa kwa ajili ya maisha mapya nje ya kazi. Wengine hujikuta hawajaweza kujenga nyumba au kuwa na biashara yoyote ya kuwaingizia fedha kwa ajili ya kuendeleza maisha yao yaliyobaki.
Msongo hutuathiri sote. Hivyo basi iwapo unaweza kutambua dalili basi unaweza kuudhibiti.
Mbali na sababu tulizoziona hapo juu, zipo sababu nyingine ambazo ni za kawaida kabisa, ambazo husababisha msongo kama kitisho, hofu na shaka.
Hofu inasababisha mtu kupatwa na msongo. Hii inajumuisha hofu ya kimaumbile, hofu ya kijamii, hofu ya kifedha na mengineyo. Katika hali ya kawaida, hali inakuwa mbaya wakati mtu anapohisi hakuna namna ya kupunguza vitisho, hiyo huathiri hisia na hivyo huwa vigumu kuzidhibiti.
Kiujumla tishio lolote katika mahitaji linaweza likasababisha msongo.
Hali yoyote ya utisho inasababisha hofu, ambayo huleta msongo. Hofu inaongoza kufikiria matokeo, ambayo ni chanzo halisi cha mawazo.
Wakati ambapo tuna shaka, hatuna uimara katika kutabiri, na wakati tunahisi hofu au tishio hali hiyo husababisha shaka.

Tabia ya utambuzi


Kunapokuwa na pengo kati ya kile tunachofanya na kile tunachofikiri, hapo tunashuhudia tabia ya utambuzi ambayo inahisiwa kama shinikizo, kwa hiyo kama ninafikiri kuwa mimi ni mtu halafu nikafanya kitu ambacho kitamuumiza mtu mwingine, hapo nitakuwa ninajiweka katika hali itakayonisababishia shinikizo.
Pengo hilo linaweza kutokea pale ambapo hatuwezi kufikia malengo yetu. Tunaamini kuwa waaminifu na tumejitoa kikamilifu lakini inapotokea jambo la kutukwamisha tusifikie malengo yetu hayo tunakumbana na mazingira yanayotufanya tuonekane kuwa si waaminifu au wenye uwezo wa kile tulichopanga kukifanya.
Mfano ni pale ambapo tunakumbana na tishio la kijamii, kwamba tusipofanya kitu Fulani, jamii haitatuelewa au tutataabika.

Chanzo kitokanacho na maisha

Kuna vyanzo mbalimbali vya msongo wa mawazo katika maisha ikiwa ni pamoja na kifo cha mume, mke, ndugu katika familia au rafiki wa karibu. Afya pia inaweza kuwa chanzo, hasa pale ambapo unahisi hali si nzuri katika mwili wako, ama kwa ugonjwa na ujauzito kwa mwanamke.
Uhalifu pia ni mojawapo ya mambo yanayoweza kusababisha msongo. Uhalifu kama vile kudhalilisha wengine kijinsia, kuvunja na kuiba, kudokoa au wizi wa mifukoni.

Kutumia dawa za kulevya

Katika ulimwengu wa sasa, watu wengi na hasa vijana, wamejikuta wakikumbwa na msongo kutokana na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, hali ambayo inawafanya kutojithamini au kukata tamaa ya maisha.
Dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia humfanya mtu ashindwe kujikinga na hatimaye kujikuta akijeruhiwa.
Mambo mengine ni mabadiliko ya ghafla katika familia kama vile mume na mke kutengana, kupata mtoto bila ya kutarajia hasa kwa wanawake walio katika ndoa.

Matatizo ya kimahusiano

Kila mtu hupenda kuwa na mahusiano ili kuoyesha ni jinsi gani anapendwa au kupenda.
Inapotokea kuwa hitaji la mtu katika mahusiano halikufikiwa, basi mtu hujikuta katika msongo ambao huathiri zaidi hisia,
hili linaweza kuwa pia katika upande wa mahusiano mabaya na mpenzi wako, mwenzi wako, rafiki au ndugu katika familia, hata mfanyakazi mwenzako au bosi katika maeneo ya kazi.
Mabadiliko ya kimaumbile; kama kukosa usingizi na kuongezewa muda zaidi kazini, mtu kuwa mnene au mwembaba au hata kurefuka au kuwa mfupi isivyo kawaida, ni baadhi ya mambo yanayochangia msongo.
Mabadiliko ya kimazingira kama vile kuhamishwa eneo la kazi au makazi, mfano kutoka mjini kwenda maeneo ya shambani, kuhama shule na kwenda katika shule ambayo hupendezwi nayo huweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kukumbwa na msongo.
Jambo jingine ni kuzidiwa na majukumu kama vile kuongeza ukubwa wa familia huku kipato kikiwa kidogo au kujikuta wategemezi wako wakiongezeka kwa ghafla, mfano watoto wa ndugu yako kuhamia kwako baada ya ndugu huyo kufariki yeye na mwenzake.

Msongo katika maeneo ya kazi

Nchini Uingereza, Idara ya Afya na Usalama inaorodhesha mambo sita makubwa ambayo yanachangia msongo katika maeneo ya kazi.
Hitaji la kazi: Udhibi walio nao wafanyakazi juu ya kazi wanazofanya na jinsi wanavyopaswa kuzifanya.
Uungwaji mkono unaoupata kutoka kwa wenzako na wakubwa wako. Mahusiano baina ya mtu na mwenzake, iwapo watu wanatambua wajibu wako na majukumu uliyonayo, na pia ni kwa kiasi gani kampuni inashauriana na wafanyakazi kuhusiana na mabadiliko ya maeneo ya kazi.
Tukutane wiki ijayo.

lcyngowi@yahoo.com
0713 331455; 0733 331455
Mwisho

Watoto Bomba; Kitabu kinachogusa mikasa na maisha ya watoto.

*ni mahsusi kwa watoto wanaoelekea kubalehe.
*Femina Hip kutawanya nakala 90,000 kwa vijana .


WATOTO wanaokulia kwa kulelewa katika mazingira mazuri wakawa na Afya njema hujenga Taifa bora na imara la baadaye katika nchi yoyote ile duniani,

Lakini ikiwa taifa lolote litakosa watoto wenye afya bora na malezi mazuri ni ukweli kwamba litakuwa linaelekea kuangamia kwani viongozi waliopo punde watakapozeeka atakosekana mrithi.

Kama ambavyo viongozi wetu wamekuwa wakisisitiza kuwa wataleta maisha bora kwa kila mtanzania ni ukweli usiopingika kwamba mkakati huo utafanikiwa ikiwa utaanzia kwa watoto.

Kwani wanahitaji kupata elimu ya kutosha ili kujenga Taifa bora na la badaye, kama hawatalelewa katika mazingira ya kupata elimu kamwe hawataweza kujenga taifa la kesho.

Mtoto anahitaji kupata elimu na kusoma vitabu mbalimbali ili kumjengea mtoto uwezo mzuri wa kufikiri na kupanua akili yake na kufahamu mambo mengi yanayohusu maisha na kujengwa katika mazingira bora yatakayomsadia hata kipindi cha mabadiliko ya mwili kuyalewa na kujua jinsi ya kukabiliana nayo.

Watoto ambao wako katika rika la kupevuka maisha yao huwa hatarini kwani mara nyingi huwa watu wanaopeda kujaribu mambo na hujikuta bila kujua wakianza vitendo vya ngono katika umri mdogo jambo ambalo hupelekea kuharibikiwa, kama wasipopata elimu ya kutosha hupata Mimba na wengine kuambukizwa virusi vya ukimwi.


Mama regina Lowassa akimsikiliza mtoto mwenye ulemavu Abudul Saleh marufu kama ‘Kapeto’ siku ya uzinduzi wa kitabu hicho ,Karimjee.


Hivi karibuni Mpango wa Elimu ya Afya Femina HIP ulizindua kitabu cha watoto kinachojulikana kama ‘watoto bomba’ kinacholenga kumweka mtoto wa kitanzania katika mazingira salama hivyo kuongeza maisha yake ya siku za usoni.

Siku ya uzinduzi wa kitabu hicho mamia ya watoto walihudhuria katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam kushuhudia kwani kinalenga kumweka mtoto wa kitanzania katika mazingira salama hivyo kuongeza ubora wa maisha yake ya kila siku.

Mama Regina Lowassa, Mke wa waziri mkuu ambaye alizindua kitabu hicho baada ya kukisoma alikuwa na haya ya kusema “mimi nikiwa kama ilivyo kwa wengine niliwahi kuwa mtoto kama walengwa wanaozungumziwa katika kitabu hiki ambacho nakizindua leo sasa basi kitabu hiki kichapishwe na kusambazwa kwa wingi”

Akionyeshwa kufurahishwa nacho alisema kuwa anakumbuka baadhi ya matatizo yaliyoelezwa kwenye kitabu hicho na yeye aliyapitia alipokuwa mtoto pia hata baada ya kukua na kuanza kupata watoto aliona changamoto mbalimbali zitokanazo na mabadiliko ya kimwili na kiakili ambazo watoto hukabiliana nazo.

Anasema kuwa kama yalivyo makundi mengine,watoto wana haki ya kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na masuala yanayowazunguka hivyo kuwafanya waishi katika mazingira ya furaha na yenye kujaa matumaini kwa siku za usoni.

Katika kitabu hicho kuna simulizi za maisha ya Kijana Salum akitishiwa maisha na wenzake darasani ,akipigwa kwa sababu ya kuwa mtulivu na msikivu , hakupata msaada wa kutosha bali alipata ujasiri wa kushtaki kwa mwalimu na vijana wenzake wakaadhibiwa na Mwalimu.



Mama Regina Lowassa akiwa anaonyesha kitabu cha watoto Bomba juu kuashiria uzinduzi huo kukamilika katika viwanja vya Karmjee,Dar es Salaam hivi karibuni. ,Tanzania,wa tatu kushoto Donald Pembe , mwakilishi wizara ya Elimu, Iddi Ligongo, mtangazaji wa kipindi cha wataoto bomba, Rachel Mkundai , Mhariri wa kitabu cha watoto Bomba,



Katika mfano huo tunajifunza kuwa ni dhahiri mazingira yanayowazunguka watoto wetu ni ya hatari,kuna vijana wakorofi na wababe kwa wenzao kwa hiyo ni jukumu la kila mmoja katika nafasi yake awe Mwalimu,Mzazi au Serikali ili kuwalinda vijana.

Pia kitabu hicho kinazungumzia tatizo la ulemavu ambalo lipo kwenye jamii yetu ,kwa mfano ukisoma habari ya mtoto abdallah Saleh iliyomo ndani ya kitabu hicho inaonyesha jinsi ambavyo watoto wenye ulemavu walivyo na tabia kama walivyo watoto wasio na ulemavu.

Kitabu hicho kinaeleza kuwa watoto wote wa kike na kiume hawajui ukweli kuhusu mabadiliko yanayotokea katika miili yao katika ukuaji wao, kutokana na vijana hawa kutoandaliwa na wazazi au walezi jinsi ya kukabiliana na mabadiliko haya.

Mama Regina anaonya kuwa watoto wengi wamekuwa wakipewa taarifa zisizo sahihi na watoto wenzao kuwa ukivunja ungo ,unakuwa na uwezo wa kujamiiana wanaosema hivyo hawajui kwamba kubalehe tu siyo tiketi ya kujamiiana.

Alikisifu kitabu hicho kuwa kimezungumzia vizuri suala VVU/UKIMWI na kuelezea kwa undani VVU inaambukizwaje,jinsi ya kujikinga na jinsi ya kuishi na mtu mwenye VVU.

Kutokana na umuhimu wa kitabu hicho hasa kwa watoto wa mashuleni Mama Regina amewaomba Femina HiP kuchapisha nakala nyingi zaidi ya 90,000 walizokuwa wamedhamiria kuchapisha ili watoto wengi waweze kufaidika nacho, kwani nakala hizo ni chache ikilinganishwa na idadi ya watoto hapa nchini.

“Kwa upande wa serikali ninaomba iendelee kuboresha maisha ya watoto wa Tanzania ili tuweze kupata Taifa bora la kesho, maana watoto hawa wakipata mwongozo thabiti ni dhahiri kwamba ile dhana ya Maisha bora kwa Kila Mtanzania itawezekana ! Maisha Bora kwa kila Mtanzania huanzia kwa watoto’ alisema Mama Regina

Akikielezea Kitabu hicho Mhariri wake Rachael Mkundai alisema kuwa ‘Watoto Bomba’ ni kitabu kilichojaa simulizi za watoto wa kitanzania , michoro na picha za kusisimua.

Kitabu cha watoto bomba ambacho watoto wengi walishiriki kusimulia hadithi zao wameonyesha uzoefu wao katika matukio wanayokumbana nayo na wakatoa maoni kitakuwa kinagawiwa bure kwenye vituo vya watoto popote pale nchini.

Rachel anasema simulizi na hadithi za picha zilizomo kwenye kitabu hicho ni za kweli tena zinafaa kuwafundisha watoto kuhusu mabadiliko ya mwili hasa wakati wakubalehe na kuvunja ungo kwa kuwa wakati huu,

Ni changamoto kubwa kwa maisha ya mtoto na kitabu hicho kinajibu maswali , hisia na wasiwasi alionao mtoto na kumpa ukweli kuhusiana na hatua ya kukua.

Ndani ya kitabu hiki mtoto atasoma kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika maisha ya kila siku nakupata ushauri wa jinsi ya kukabiliana nazo .

Pia watoto watakaokisoma watajifunza jinsi ya kushirikiana na watu wazima na watoto wenzao ili kutatua matatzo katika familia zao na jamii wanayoishi.

Watoto watapata mbinu za kupambana na uonevu na jinsi ya kutatua matatizo kwa njia zisizo na vurugu , jinsi ya kuutambua na kuuukabili ulemavu wa aina mbalimbali kuishi na VVU na UKIMWI.

Mambo mengine yaliyomo katika kitabu hiki kitampa mtoto uwezo wa kuutambua unyanyasaji wa kijinsia , kuishi kwa usalama yakiwemo mambo ya usalama barabarani ,

utoaji wa huduma ya kwanza katika matukio mbalimbali kukabiliana na mabadiliko kama sehemu ya maisha,

haki na wajibu wa mtoto katika jamii.na kila mwisho mwa kila sura kuna safu ya wakufunzi kwa ajili ya walimu ili kuwasadia watoto jinsi ya kutumia kitabu hiki.

Kabla ya kuchapishwa kwa kitabu hicho kilipitiwa na wadau mbalimbali wakiwamo watoto wenyewe na kutoa michango yao ambayo imejumuishwa katika kitabu ili kuboresha maudhui yake.

Baadhi ya wadau hao ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi , Mradi wa Vitabu vya Watoto , Plan International, Kiwahede na CCBRT na wengine wengi.


Baadhi ya watoto walishiriki ili kukamilisha kitabu hicho ni pamoja wanafunzi wa Shule ya Msingi Maktaba ya jijini Dar es Salaam, Shule ya msingi Miswe ya mjini kibaha ,Chanzige kutoka Kisarawe ,kikundi cha sanaa cha shada kutoka Bagamoyo na kikundi cha watoto toka Kigamboni.

Pia walemavu walishirikishwa kutoka shule za walemavu jeshi la wokovu , Uhuru mchanganyiko ,Mtoni maalum,vitengo vya watoto wenye ulemavu katika shule za Msingi Mtoni na Tandika zote za jijini Dar es Salaam pamoja na kikundi cha watoto yatima wanaoishi na VVU (TOCHA+)

“Watoto wa kitanzania ndio watakao tengeneza Tanzania ya baadaye tunawashukuru wote kwa kutuunga mkono na kushirikiana nasi katika kazi hii ,ni matumaini yetu kitabu kitawaelimisha na kuwaburudisha pia” alisema Rachel ambaye ni mhariri wa kitabu hicho.

Anasema kuwa nakala nyingi zitategea wafadhili watakaojitokeza ni matumaini ya wengi kuwa wafadhili watauitikia wito huo ili nakala nyingi ziweze kuchapishwa na watoto waweze kukipata.

Sunday, November 4, 2007

Mstaafu EAC afariki akifuatilia mafao Dar

*Asotea miaka minne jijini bila mafanikio

Na Grace Michael

MSTAAFU wa lililokuwa Shirika la Reli la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Laston Mwakabana, mkazi wa Kyela, Mbeya, ambaye alikuwa Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia mafao yake, amefariki dunia.

Akizungumza katika ofisi za gazeti hili jana, mstaafu mwenzake, Bw. Malugu Musa, ambaye naye yupo jijini kufuatilia mafao hayo, alisema Bw. Mwakabana alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Bw. Mussa alisema marehemu alianza kutapika na kuharisha damu na alimpeleka Hospitali ya Amana Jumapili usiku, na baadaye alihamishiwa Muhimbili wodi ya Sewa Haji namba 24 Jumatatu asubuhi ambako aliongezwa damu.

Alieleza kuwa marehemu amekuwa akifuatilia mafao yake jijini kwa miaka minne bila mafanikio huku akiwa ameweka makazi yake katika stesheni ya treni.

Kupitia taarifa hii, Bw. Mussa aliomba ndugu na jamaa wa marehemu Mwakabana kutoka Kyela na kwingineko, wajitokeze kuuchukua mwili wa ndugu yao na kwenda kuuzika.

Alisema kwa anayehitaji kupata taarifa zaidi za msiba huo, awasiliane na Bibi Edah Itende wa TRL, Dar es Salaam kupitia namba 0754 675930.

Alisema wao wakiwa wafuatiliaji wa mafao hayo wamesikitishwa na msiba huo kwani marehemu alikuwa mstari wa mbele kufuatilia haki zao bila kuchoka. Marehemu alizaliwa Lubaga, Bujonde Mission, Kyela.
.07.2006 0954 EAT

Baada ya kupokea mafao yake...Mwalimu mstaafu afia gesti

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

MWALIMU mstaafu aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kuchukua mafao yake amekufa baada ya kumeza vidonge viwili vya Aspirin akiwa katika nyumba ya kulala wageni mjini Kahama mkoani hapa.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Simon Sirro, alimtaja mwalimu huyo kwa jina la Bw. Ngereja Taratibu (60) mkazi wa kijiji cha Ushetu wilayani Kahama mkoani hapa na kwamba tukio hilo lilitokea Julai 16 mwaka huu saa 8.30 usiku.

Akifafanua, Kamanda Sirro alieleza kuwa siku ya tukio mwalimu huyo akiwa ameongozana na mkewe wakitokea Dar es Salaam, walifika mjini Kahama na kupanga chumba katika nyumba ya kulala wageni ya Magasa.

Alisema siku ya tukio wanandoa hao walikwenda baa kujiburudisha kabla ya kujipumzisha wakisubiri safari ya kurejea kijijini kwao siku ya pili yake.

Kamanda alisema baadaye walirejea katika nyumba ya wageni walimofikia na usiku Bw. Taratibu alijisikia maumivu makali kifuani hivyo aliamka na kuchukua vidonge hivyo na kuvimeza ili kupunguza maumivu.

Mara baada ya kumeza vidonge hivyo, Bw. Taratibu alianguka chini na kufariki dunia.

Kamanda alisema hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo na Polisi inaendelea na uchunguzi wa kina juu ya kifo hicho.

Katika tukio lingine, mkazi wa kijiji cha Kibeshi, tarafa ya Dutwa wilayani Bariadi, amekutwa amekufa baada ya kupigwa na kito kizito kichwani.

Kamanda Sirro alimtaja mkazi huyo kuwa ni Bw. Sitta Seni (30) na kwamba tukio hilo lilitokea Julai 13 mwaka huu saa 11 jioni.

Alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Bw. Seni inadaiwa alipigwa na kitu kizito kichwani na Bw. Chenye Ponoku, ambaye alimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe.

Bw. Ponoku ambaye baada ya tukio hilo alitoweka, hivi sasa anasakwa na Polisi.
25.04.2006 1055 EAT

Mstaafu EAC adai hundi yake imetoweka Hazina

Na Said Mwishehe

MSTAAFU wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bw. John Herbert, amedai mafao yake yamepotelea Hazina katika mazingira ya kutatanisha, kutokana na kukuta hundi yake imesainiwa na mtu asiyemfahamu.

Bw. Herbert ambaye wakati wa EAC alikuwa akifanya kazi Shirika la Reli Tanzania (TRC), amedai alifika Hazina, lakini alishangaa kuona nyaraka zinaonesha kuwa ameshasaini na kuchukua hundi wakati hajafanya hivyo.

Akizungumza katika ofisi za gazeti hili mapema wiki iliyopita, mstaafu huyo alidai baada ya kukamilisha taratibu zote za ufuatiliaji mafao Februari mwaka jana alitakiwa kwenda kuchukua hundi yake, lakini baada ya kufika Hazina ndogo iliyopo eneo la Posta ya Zamani, Dar es Salaam, aliambiwa kuwa tayari imeshachukuliwa.

"Nimeshangaa kuona naambiwa tayari hundi yangu imechukuliwa na ukiangalia sijawahi kufika hapo na kusaini hundi hiyo, hivyo naamini kuna baadhi ya watu wa Hazina wamefanya ujanja ili wanidhulumu mafao yangu," alilalamika Bw.Herbert.

Alisema kibaya zaidi ni pale anapokwenda kufuatilia hatima ya kujua haki yake ya malipo ya mafao katika ofisi ndogo ya Hazina, na kufukuzwa baadhi ya wafanyakazi wakionehs kana kwamba hapaswi kufahamu kinachoendelea.

"Nashindwa kuelewa kinachoendelea, kwani kila ninapokwenda Hazina ndogo, naambiwa niondoke na suala langu linafanyiwa kazi, sasa sielewi kinachoendelea na taarifa za utata huo nilishatoa Hazina kuu tangu Januari mwaka huu,"alisema Bw.Herbert.

Bw. Herbert alidai kwamba utata huo umemfanya azidi kuwa katika hali ngumu kimaisha, kwani baada ya kukamilisha taratibu za mafao yake, alikopa pesa kwa watu mbalimbali kwa lengo la kujikimu kimaisha, huku akijua kwamba atazirejesha baada ya kuchukua mafao yake.

"Nimekopa fedha nyingi kutoka kwa watu nikiamini nitarudisha, pia nilichukua fedha kwa ajili ya nauli ya kunileta Dar es Salaam kutoka mkoani Tabora ambako ndipo naishi na familia yangu," alilalamika Bw.Herbert.

Bw.Herbert ambaye namba yake ya kazi ilikuwa ni 668859 alianza kazi mwaka 1968 na kustaafu mwaka 1979 mkoani Tabora.

Hata hivyo gazeti la Majira baada ya kufuatilia suala hilo Hazina ndogo kwa lengo la kupata ukweli, baadhi ya maofisa waliokuwa zamu walisema wenye uwezo wa kuzunguzia suala hilo ni Hazina kuu.

Majira lililazimika kwenda Hazina kuu ambako ofisa habari wa Hazina kuu aliyejitambulisha kwa jina moja la Bi. Mbuya alisema anayeweza kuzungumzia habari za mafao ni Mhasibu Mkuu wa Serikali.

Majira ilipokwenda katika ofisi ya Mhasibu Mkuu, iliambia alikuwa kwenye kikao, lakini hata hivyo waliokuwapo hapo walisema anayepaswa kujibu suala hilo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.

Kutokana na danadana hizo, Majira ilirudi kwa Ofisa Habari ambaye aliomba aachiwe maswali ayakabidhi kwa Katibu Mkuu ili ukweli ufahamike.

Wahisani walia na rushwa

na Ratifa Baranyikwa

WADAU wa maendeleo nchini wamesisitiza kuwa vita dhidi ya rushwa ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele kivitendo na matokeo yake yanapaswa kuonekana kwa vitendo.
Hayo yamo kwenye tamko lao walilolitoa jana wakati wakihitimisha mjadala uliodumu kwa muda wa wiki moja wa mapitio ya bajeti ya mwaka 2007, lililosomwa na Mwenyekiti wa kundi la wadau wa maendeleo, David Stanton.
“Mtazamo wa wadau wa maendeleo, ambao tumeshirikiana na serikali kupitia mjadala huu tumeafikia masuala matano kuhusiana na bajeti ya mwaka huu, ambayo ni uhitaji wa kuonyesha na kuwasilisha matokeo, pili kuna umuhimu wa hali ya juu katika kupambana na rushwa kujenga maendeleo ya kisasa,” alisema.
Aidha, alisema kuwa pamoja na kuridhishwa na maeneo mengi yanayoonyesha maendeleo, lakini kuna uhitaji wa ushahidi wa matokeo na masuala ya rushwa katika maeneo hayo.
“Tumekuwa na mapitio ambayo yamezaa matunda, tumeeleza kuridhishwa na maendeleo ya maeneo mengi, lakini tuko makini sana na uhitaji wa ushahidi wa matokeo na rushwa katika maeneo hayo,” alisema.
Akisoma tamko hilo, Stanton alisema kuwa pia wadau hao wako makini sana na udhaifu wa uwazi katika pesa za serikali za mitaa, hasa kuhusiana na usahihi wa taarifa za matumizi ya fedha zilizopo katika bajeti.
Alisema kuna ulazima wa kuwa na uwazi hasa katika pesa zinazokwenda kwenye wilaya na kusisitiza kuwa matokeo ya bajeti yaweze kuonekana kwa kuonyesha mabadiliko kutokana na kazi itakayofanywa na fedha hizo.
Aliwaambia watu ambao walihudhuria mkutano huo, katika kipindi chote walichokuwa wakipitia bajeti, kumekuwa na mjadala wa wazi kuhusiana na masuala ya rushwa na kwamba wamekubaliana na serikali kuhusiana na suala la kuwa na uwazi katika mapambano ya rushwa, hivyo wanatarajia mwitikio wa serikali katika kuimarisha matokeo ambayo yamepatikana.
Pia, alisema kuwa kulikuwa na makubaliano juu ya uhitaji wa mpango wa utekelezaji wa mkakati wa maendeleo kutoka wachangiaji wa bajeti na sekta binafsi, wasomi, wadau wa maendeleo kutoa mpango ulio sahihi wa maamuzi ya kiuwekezaji katika kutetea masilahi ya serikali hasa katika upande wa rasilimali.
“Tatizo hilo tumeliangalia, na hii inafanyika sana kwenye maeneo ya rasilimali ambako udhaifu wa utawala na matumizi ya rushwa ni makubwa, kitu ambacho kinasababisha kupoteza kodi nyingi za serikali,” alisema.
Aidha, alisema kuwa wadau wa maendeleo wako tayari kuisaidia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwenye upande wa rasilimali.
Pia alisema kuwa kuna haja ya kuchukua hatua ili kuboresha huduma muhimu katika rasilimali watu.
Naye Profesa Samuel Wangwe, ambaye ni mshauri wa masuala ya uchumi wa serikali, alisema kuwa mjadala huo ulikuwa mkali sana.
Alisema kuwa baadhi ya vitu ambavyo walivijadili ni pamoja na rasilimali watu, ikiwa ni pamoja na kutengeneza nafasi za kazi katika kiwango ambacho kinakubalika.
Alisema kuwa suala la utawala bora nalo lilikuwa moja kati ya agenda katika mjadala huo ili kuhakikisha kuna kuwa na uwazi.
Profesa Wangwe alisema kuwa masuala ya rasilimali, uingizaji wa bidhaa nchini na kodi pia lazima yafanyike kwa uwazi.