Friday, May 25, 2007

तंजानिया यजिटिया KITANZI

Shirika la Afya Duniani (WHO) lafafanua msimamo wake juu kupunguza matumizi ya DDT kupambana na malaria

*Dunia yatakiwa kuamka kuhusu DDT: Uzalishaji na matumizi vyaongezeka kufuatia kusainiwa kwa Mkataba wa Stockholm, Tanzania yazidi kupata wakati mgumu kuitumia.



Na Mobini Sarya



Aprili 25 mwaka huu ilikuwa Siku ya Malaria Barani Afrika , kauli mbiu ya siku ya malaria mwaka huu (2007) ni ''Ondoa Malaria Afrika Sasa'' na ujumbe “Uongozi na Ushirikiano kwa Matokeo," serikali ilielezea mipango yake katika kukabiliana na ugonjwa huo. Mipango hiyo inahusisha matumizi ya dawa mpya ya kutibu malaria ya ALU, na kutumia DDT (DDT - Dichloro-dipheny-trichloroethane) kwa ajili kunyunyizia ndani ya nyumba kudhibiti mbu waenezao malaria.


Malaria ni ugonjwa unaotishia maisha unaoenezwa na mbu kwa njia ya vijidudu (parasite) vijulikanavyo kama plasmodium ambavyo vinaenezwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu jike aina ya anofelesi (anopheles). Mbu aina hii hutumia damu kwa ajili kukuzia mayai yake.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa malaria unawapata watu zaidi ya milioni 300 na wastani wa vifo milioni moja kila mwaka, kiasi cha 80% kati ya vifo hivyo vikitokea barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, na wengi wao wakiwa ni watoto chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito na watoto ambao bado hawajazaliwa.



Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inakadiria kuwa wastani wa watu 100,000 nchini Tanzania hufa kwa malaria kila mwaka. Ugonjwa huu ni hatari kwa afya na una athari kubwa kiuchumi kutokana na gharama za matibabu na muda wa kazi uliopotea kwa wagonjwa na kuwahudumia.


Wiki moja baada ya maadhimisho hayo, ulifuatia Mkutano wa Tatu wa nchi ridhia wa Mkataba wa Kimataifa wa Stockholm kuhusu kemikali za sumu zinazodumu na kuendelea kuleta madhara kwa binadamu na mazingira kwa muda mrefu (POPs - persistent organic pollutants), uliofanyika huko Dakar, Senegal kuanzia tarehe 30 Aprili mpaka 4 Mei 2007. Tanzania katika mkutano huo iliwakilishwa na serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mazingira na mashirika na taasisi zisizo sa Serikali zinazofanya kazi zinazohusiana na uhifadhi wa mazingira na kemikali.



Moja ya dondoo kubwa za Mkutano huo ilikuwa ni matumizi ya DDT katika kudhibiti malaria.

Serekali zilizoshiriki katika Mkutano wa Tatu wa nchi ridhia kwa Mkataba wa Kimataifa wa Stockholm uliofanyika Dakar, Senegal kati ya tarehe 30 Aprili na 4 Mei 2007 kuhusu kemikali za sumu zinazodumu na kuendelea kuleta madhara kwa binadamu na mazingira kwa muda mrefu (POPs - persistent organic pollutants) zilishangaa kusikia kuwa uzalishaji na matumizi ya DDT yameongezeka tena, licha ya Mkataba huo kuzuia kwa lengo la kuiondoa kabisa.

Wanachama wa Mtandao wa mashirika ya kiraia juu ya viuatilifu (Pesticide Action Network - PAN) na Mtandao wa kuondoa POPs duniani (International POPs Elimination Network - IPEN) walioshiriki katika mkutano huo walitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendeleza dhamina na ahadi ya kutokomeza malaria katika bara la Afrika na penginepo duniani kwa njia mbadala zisizotumia DDT.

“DDT ni tatizo katika karne ya 21 duniani kote,” alisema Henry Diouf, kutoka mtandao wa mashirika ya kiraia juu ya viuatilifu barani Afrika (PAN Africa). “Nchi zote zinatakiwa kuchukua hatua za haraka kuhusu tatizo hili sasa.”

Mkataba wa Stockholm uko wazi kabisa kuhusu DDT: Unatoa ruhusa maalum kwa matumizi tu ya kupambana na visumbufu vya magonjwa katika sekta ya afya, ukiwa na lengo la kuipunguza na hatimaye kuiondoa kabisa. Katika Mkutano huo wa Tatu wa nchi ridhia, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisisitiza kuunga kwake mkono malengo ya Mkataba huo na kuelezea kuguswa kwake na madhara yatokanayo na DDT kwa afya ya binadamu.

Etekelezaji thabiti wa Mkataba huo unahitaji kiasi cha kutosha cha fedha na utaalamu na mifumo inayowezesha utekelezaji katika ngazi ya kitaifa. Kiasi cha dola za Marekani milioni 300 (shilingi za Tanzania 375 bilioni) zimetengwa kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa ajili kuwezesha nchi zinazoendelea zilizoridhia Mkataba huo kudhibiti uingiaji wa kemikali hizo za POPs katika mazingira.

Kuna changamoto nyingi zinazozikabili nchi zinazoendelea katika kutimiza wajibu wake aktika Mkataba wa Stockholm. Changamoto hizo ni pamoja na njia thabiti za kudhibiti malaria bila kutumia DDT, njia za kusimamia na kushughulikia taka za sumu pasipo kuleta madhara, na mbadala wa teknolojia zinazochangia uchafuzi wa mazingira. Inaeleweka kuwa pasipo kuongeza kiasi cha fedha, gharama za kutekeleza Mkataba huo utazidi uwezo wa nchi nyingi zinazoendelea.

“Nchi zinazoendelea haziwezi kutekeleza Mkataba wa Stockholm kikamilifu pasipo kupata misaada ya kutosha ya kifedha na kitaalamu,” alisema Profesa Jamidu Katima, Mwenyekiti mwenza wa mtandao wa kuondoa POPs duniani (IPEN) na Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika mwanachama la AGENDA la Tanzania, AGENDA ni mwanachama wa IPEN na PAN.

Mashirika ya IPEN na PAN pia yalisisitiza kukataa viwango duni vilivyopendekezwa kwa muda kwa ajili ya kusimamia taka za POPs na zile zenye mchanganyiko wake. Mwongozo uliokubaliwa haukuzingatia viwango vya kulinda afya na hivyo kuweza kuruhusu uingizaji wa kemikali za sumu zilizochanganyika na taka za POPs katika nchi zinazoendelea.

Wiki iliyopita wakati Mkutano wa tatu wa nchi ridhia za Mkataba wa Kimataifa wa Stockholm juu ya POPs (POPs ni kemikali za sumu ambazo hudumu katika mazingira na kuendelea kuleta madhara ya kiafya na mazingira muda mrefu baada ya kutumika) uliofanyika huko Dakar, Senegal, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Ofisi ya Afya na Mazingira Dk. Maria Neira alisisitiza kuwa Shirika la Afya Duniani linaunga mkono Mkataba huo wa Stockholm, na kwamba linadhamiria kupunguza utegemezi wa matumizi ya DDT katika kupambana na malaria.

Akiongea na sehemu kubwa ya wajumbe wa Mkutano huo katika mjadala ulioandaliwa na Shirika la Afya Duniani kwa kushirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kuhusu “Kupunguza utegemezi wa DDT na kuimarisha kampeni ya kupambana na malaria,” Dk. Neira alisisitiza lengo la Shirika la Afya Duniani kupunguza matumizi ya DDT na hatimaye kuiondoa kabisa kulingana na Mkataba wa Stockholm. Aliongeza kuwa huo ndio msimamo wa Shirika tangia kusainiwa kwa Mkataba huo, na msimamo huo haujawahi kubadilika.

Dk. Neira pia alithibitisha kukubaliana kwa Shirika hilo na madhara ya kiafya yanayosababishwa na DDT, kwamba “Shirika linatambua na kuguswa na madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya DDT.” Aliongeza kuwa “Shirika limedhamiria kupata mbadala wa DDT mapema iwezekanavyo” na kuhakikisha mataifa wanachama yanazingatia masharti yaliyowekwa juu ya matumizi ya DDT na kutoa taarifa za matumizi yake.

WHO na UNEP walitangaza kuwa tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Stockholm, matumizi ya DDT yameongezeka mara mbili. Nchi nyingi bado zinatumia DDT kwa ujumla bila kuchagua maeneo yaliyoathirika kiasi cha kulazimika kunyunyiziwa kama ulivyo muongozo wa Shirika la Afya Duniani. Hii inatokana na upungufu wa fedha na utaalamu katika nchi nyingi zinazokabiliwa na tatizo la malaria.

Shirika la afya Duniani pia limeweka wazi kuwa unahitajika msaada mkubwa wa kifedha kutoka nchi zote ili kukabiliana na malaria kwa kutumia mbinu zinazohusisha programu mchanganyiko za udhibiti wa visumbufu (vijidudu), na kupunguza matumizi ya DDT.

Haja ya kuwekeza katika kujenga uwezo ilisisitizwa mara kadhaa katika mjadala huo wakati wa kuwasilisha mada. Wakati mwakilishi kutoka Ujerumani alipotamka kuwa zinahitajika Euro milioni 10 (sawa na zaidi ya shilingi bilioni 17 za Tanzania), alitakiwa na Shirika hilo (WHO) kuongeza kiwango hicho kufikia Euro milioni 50 (sawa na shilingi bilioni 86 za Tanzania).

Msemaji wa UNEP alisisitiza kuwa mbinu mchanganyiko za kudhibiti visumbufu vya afya ndizo zipewe kipaumbele katika juhudi za kupunguza matumizi ya DDT, yakiwepo matumizi ya viuatilifu vingine kama kimbilio la mwisho pale ambapo mbadala wa kemikali hautoshelezi. Dk. Lucien Manga wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika alisema shirika hilo lina sera iliyo wazi juu ya matumizi ya mbinu mchanganyiko katika kukabiliana na malaria, na kuwa mbinu hizo zinahusisha ushirikishwaji wa jamii husika; kutafuta ili kujua sababu za kuenea kwa ugonjwa huo katika sehemu fulani; na matumizi ya mkusanyiko wa mbinu nyinginezo kwa ujumla zinatakiwa kuonesha uthabiti wa mbadala wa kemikali katika nchi yenyewe.

Msemaji wa Shirika hilo (WHO) pia alisisitiza umuhimu wa kuwepo mpango kazi wa kidunia wa katika kutafuta mbadala mpya wa kemikali hizo na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi zinazoendelea.

Katika mjadala huo pia Dk. Enrique Loyola wa Shirika la Afya la Pan Amerika (Pan American Health Organization) alizingumzia juu ya mradi wa kupambana na malaria ncini Mexico ambao ulipinguza kwa kiasi kikubwa sana tatizo la malaria pasipo kutumia DDT. Alisema walifanikiwa kupunguza malaria kwa asilimia 30 (30%) katika ngazi ya vijiji na asilimia 50 (50%) kitaifa.

Njia walizotumia ni pamoja na elimu kwa umma, upandaji wa miti yenye kutoa harufu inayofukuzisha mbu karibu na nyumba za kulala na kusafisha vichaka ambavyo vinaweza kuwa mazalia au makao ya mbu, kupaka nyumba chokaa yenye uwezo wa kuwafanya mbu wakimbie, uzingatiaji wa masharti ya binafsi, kusafisha mifereji na madimbwi na kuondoa utando unaowahifadhi mbu katika maji.

Pia matumizi ya vimelea vinavyoua mbu vijulikanavyo kama Bt (Bacillus thuringiensis). Mexico kwa sasa haitumii tena DDT katika kupambana na wadudu kama mbu, na kwa sasa inapunguza pia matumizi ya kemikali nyingine katika kukabiliana na visumbufu vya afya.

Katika majadiliano yaliyofanyika baada ya uwasilishwaji mada, Dk. Basu wa viwanda vya Hindustan vya India, watengenezaji wa DDT inayotumika barani Afrika, alisema kwamba hakujawahi kutokea hata kifo kimoja au mtu aliyedhurika na matumizi ya DDT, kwa DDT iachwe iendelee kutumika. Alipomaliza tu kusema hivyo alipokelewa na miguno iliyopinga kauli hiyo kutoka katika wajumbe waliofurika katika ukumbi wa mkutano.

Dk. Neira alidakiza kuwa “Shirika la Afya Duniani linaguswa sana na madhara ya kiafya yatokanayo na DDT” na “inasikitishwa sana na matokeo ya madhara hayo ya kiafya kwa matumizi ya DDT.”

Mshiriki mmoja aliliwaambia wasemaji wa Shirika la Afya Duniani kuwa wakati mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kiraia yanaposema hivyo juu ya madhara ya DDT kwa afya, yanapuuzwa na kusemekana kuwa ni wapingaji ambao wanaishia tu kurejea taarifa za muda mrefu za Shirika hilo. Aliliomba Shirika hilo kutoa taarifa rasmi kuhusu madhara ya afya yatokanayo na DDT.

Alisema mashirika ya kiraia yapo tayari kufanya kazi na Shirika hilo katika kusaidia kupunguza tatizo la malaria, lakini yamekuwa yakikatishwa tamaa na dhana isiyo sahihi kuwa Shirika hilo la Afya linaunga mkono na kutetea kuendelea kutumika kwa DDT. Dhana hiyo ilisababishwa na tarifa iliyotolewa na Shirika hilo mwezi Septemba 2006, ambayo ni tofauti sana na msimamo uliooneshwa na Shirika hilo katika mada yake wakati wa Mkutano wa tatu wan chi ridhia za Mkataba wa Stockholm jijini Dakar, Senegal.

Dk Neira alijibu kuwa kutokueleweka kwa msimamo wa Shirika hilo kunatokana na taarifa ya hiyo ya mwezi Septemba 2006 kwa vyombo vya habari, na kwamba Mkutano wa Dakar uchukuliwe ndio msimamo rasmi wa Shirika la Afya Duniani kwa sasa kuhusu matumizi ya DDT katika kupambana na malaria, na kuwa Shirika linatambua na kuheshimu malengo ya Mkataba wa Stockholm ambayo ni kulinda afya za watu kutokana na madhara ya kemikali za POPs, DDT ikiwa mojawapo.

AGENDA ni mwanachama wa Mtandao wa mashirika ya kiraia katika kuondoa POPs duniani, IPEN (International POPs Elimination Network) na Mtandao wa mashirika ya kiraia juu ya viuatilifu PAN, (Pesticide Action Network)


website' www. mobinday.blgospot.com 0753 399 579 email;mobinsons@yahoo.com 0717 328 102.

Labels: