Wednesday, June 6, 2007

मबदिलिको या हली या hewa

SIKU ya Mzingira duniani na mabadiliko ya hali ya hewa yanavyotishia uhai wa viumbe.

Na Mwandishi wetu.

WIKI iliyopita Duniani iliadhimisha siku ya Mazingira ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni 5 siku hiyo ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1972 katika kuadhimisha ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Mazingira ya Binadamu uliofanyika Stockholm , Sweden (Stockholm Conference on the Human Environment). Siku hiyo hiyo Baraza hilo pia lilipitisha azimio la kuanzisha Shirika la Mazingira Duniani (UNEP).
Siku ya Mazingira Duniani inaweza kusherehekewa kwa namna nyingi, kama matembezi, makongamano, mashindano ya insha na michoro, upandaji miti, kazi za kurejelea vitu mbalimbali, kampeni za usafi, mijadala ya wazi, warsha na semina, vipindi katika vyombo vya habari na nyinginezo. Katika nchi nyingi, maadhimisho haya yanatumika kuhamasisha dhamira na shughuli za utunzaji mazingira.
hapa nchini maadhimisho hayo yalifanyika kitaifa mkoani Mtwara yakiongozwa na Makamu w a Rais, Dk. Ali Mohammed Shein yakiwa na kauli mbiu inayosema hifadhi Mazingira;Panda miti.
siku kama hiyo Wakuu wanchi, Mawaziri Wakuu na Mawaziri wa Mazingira hutoa taarifa, mikakati na ahadi mbalimbali za utunzaji wa mazingira. Ahadi timilifu zaidi hutolewa juu ya uanzishwaji wa vitengo au idara za kudumu za kushughulika na usimamizi wa mazingira na mipango ya kiuchumi. Maadhimisho haya pia yanatumika kama nafasi ya kusaini au kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusiana na mazingira.
Lengo kubwa la siku hiyo ni kuwapa watu nafasi ya kushughulikia masuala ya mazingira kwa kina zaidi; kuwawezesha kuwa mawakala wazuri zaidi wa maendeleo endelevu na kuhimiza na kuhamasisha uelewa kuwa jamii ndiyo ndiyo msingi wa mabadiliko ya kimtizamo juu ya masuala ya mazingira; na kuhimiza ushirikiano ambao utahakikisha mataifa yote na watu wake wanafurahia mazingira salama sasa na vizazi vijavyo.


Kauli mbiu ya siku ya mazingira duniani mwaka huu 2007 ni “Kuyeyuka kwa theluji na barafu duniani – suala linavuta kuwepo mjadala?” Ujumbe wa siku hiyo mwaka huu unalenga madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa jamii na viumbe waishio ncha za dunia, na matokeo yake duniani kwa ujumla.

Jamii inaalikwa kupambanua hali katika mazingira yao . Kuna umuhimu wa kufikiria kwa kina na uangalifu hatua ambazo kila mmoja anaweza kuchukua, na kuwa sehemu ya jukumu la kutunza uhai wa kila kiumbe katika hali ya kujali mazingira yetu.

Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira mwaka huu, Asasi ya AGENDA for Environment and Responsible Development (AGENDA) iilitoa taarifa inayoonesha uhusiano uliopo kati ya mabadiliko ya hali ya hewa, uchumi, afya na athari za kimazingira na namna vinavyoweza kukwaza juhudi na mikakati ya kupambana na umaskini.


Mabadiliko ya hali ya hewa ni tofauti kubwa inayotokea kati ya viwango vya wastani kwa vipimo vya hali ya hewa na kuendelea kwa muda mrefu. Mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kusababishwa na nguvu za asili au mabadiliko yanayotokana na shughuli mbalimbali za binadamu katika matumizi ya ardhi na kubadilika kwa mfumo wa hewa zilizoko katika anga na mazingira kwa ujumla.
MABADILIKO YA HALI YA HEWA YALIVYOBADILIKA

Mabadiliko ya hali ya hewa sasa ni dhahiri kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha wastani wa joto la hewa duniani na baharini, kuyeyuka kwa theluji na barafu sehemu mbalimbali duniani, na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari duniani. Wastani wa joto la hewa duniani umeongezeka kwa nyuzi joto 0.76° C tangu mwaka 1850. Inaaminika kuwa kiasi kikubwa cha ongezeko la joto katika kipindi cha miaka 50 iliyopita kimetokana na shughuli za binadamu.

Katika ripoti yake ya nne ya kuangalia mfumo wa mabadiliko ya hali ya hewa iliyochapishwa tarehe 2 mwezi Februari 2007, Baraza la Dunia juu ya mabadiliko ya hali ya hewa (Intergovernmental Panel on Climate Change) (IPCC) ilisema kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kupunguza gesi zinazosababisha kuongezeka kwa joto, wastani wa joto la uso wa dunia utaongezeka na kufikia kati ya nyuzi joto 1.8°C na 4.0°C katika karne hii.

Kadirio la ongezeko la joto kwa karne hii linaweza kusababisha madharamakubwa kwa binadamu na viumbe wengine, ikiwepo kuongezeka kwa kina cha maji katika bahari kwa kiwango cha sentimeta 18 na 59 na kuhatarisha maisha maeneo ya ukanda wa pwani na visiwa vidogo, na kuongezeka kwa matukio mengine makubwa kama vimbunga, mafuriko, ukame, na mengineyo.

Mabadiliko ya hali ya hewa ni wazi moja kati ya madhara makubwa ya kimazingira, kijamii na kiuchumi yanayoikabili dunia kwa sasa.

SABABU ZA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

Shughuli za binadamu zinazochangia mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la joto duniani zinajumuisha matumizi ya mafuta ya kuendeshea mitambo, magari na kuzalisha umemehe, shughuli za kilimo na matumizi ya ardhi kama ukataji misitu. Shughuli hizi zinasababisha kuongezeka kwa hewa ya ukaa (carbon dioxide - CO2), gesi kuu katika muchangia mabadiliko ya hali ya hewa, pamoja na gesi nyingine ('greenhouse' gases). Gesi nyingine muhimu katika kundi hilo ni gesi ya metheni (methane - CH4), itokanayo na mkandamizo wa vitu vya oganiki (vinavyooza), gesi ya ozoni (ozone - O3) na gesi nyingine ni nitrous oxide (N2O).

Gesi zinazosababisha ongezeko la joto na mabadiliko ya hali ya hewa (greenhouse gases) ni kati ya gesi zinazojumuishwa katika anga, zikiwa katika uasili wake au kutokana na shughuli nyinginezo, ambazo zinasharabu na kutoa miali ya joto. Gesi hizi huongezeka sana kutokana na uchomaji mafuta, makaa ya mawe na gesi katika mitambo, magari na kuzalishia umeme, na pia katika ukataji au uchomaji misitu na katika kilimo. Mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha kuongezeka kwa dhoruba, mafuriko na ukame, kuyeyuka kwa theluji na barafu, kuongezeka kwa kina cha maji baharini, kubadilika kwa mifumo ya hali ya hewa na kuenea kwa magonjwa.

Mabadiliko ya hali ya hewa, pia yamesababisha kutoweka kwa mito , kutoweka kwa baadhi ya viumbe na misitu muhimu iliyokuwa chanzo cha mvua.
ATHARI ZA MABADILIKO YA HAKI YA HEWA TANZANIA

Kuyeyuka kwa theluji juu ya Mlima Kilimanjaro katika kipindi cha miaka 50 iliyopita kunadhihirisha kuwa moja ya vivutio vya asili vikubwa duniani vinatoweka kwa kasi kkubwa. Inakadiriwa kuwa katika kiwango cha kuyeyuka cha sasa, theluji katika Mlima huo mrefu kuliko yote Afrika itakuwa imeisha kabisa ifikapo mwaka 2020.

Nchini Tanzania, vipimo vya hali ya hewa vimeonesha kuongezeka kwa joto kwa watani wa nyuzi joto 0.2oC kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita, na nyuzi joto 0.6oC katika nyanda za juu kusini pamoja na kupungua kwa mvua. Athari nyingine ni kuibuka na kuongezeka kwa ugonjwa wa malaria katika maeneo ambayo awali hayakuwahi kukumbwa na ugonjwa huo, mfano nyanda za juu kaskazini na kusini (Arusha, Kilimanjaro, Kagera, Mbeya and Lushoto in Tanga among others). Pia kuongezeka kwa kina cha maji baharini kulikosababisha kuzama kwa visiwa vidogo baharini na muingiliano wa maji bahari katika visima vya maji baridi.

Kwa upande mwingine, kupungua kwa mvua na mabadiliko ya viwango vya joto kumechangia kuibuka kwa aina tofauti za wadudu na pia kujenga usugu kwa kemikali zilizotumika awali kuwaua hivyo kusababisha mavuno duni katika kilimo. Halii hii imesababisha wakulima kutumia kemikali nyingi zaidi kuanzia mbolea za viwandani, kemikali za kuangamiza magugu na wadudu waharibifu katika harakati za kuongeza mazao. Nyingi kati ya kemikali hizo zina sumu kali, zinazotishia afya ya binadamu na mazingira. Pia kemikali hizo ni ghali katika gharama ya kununua na pia katika unyunyizaji mashambani. Zinaua pia viumbe muhimu katika kulaininisha na kuruhusu hewa na maji kupenya katika udongo ambavyo ni muhimu katika kukuza mazao.

Kuibuka, kuongezeka kwa malaria na usugu wake katika maeneo yaliyotajwa pia kulifanya serikali na mashirika mbalimbali kuanza kunyunyizia kemikali tofauti kwa ajili ya kuua mbu wa malaria, moja ya kemikali hizo ikiwa ni DDT. DDT ni moja kati ya kemikali za sumu zenye tabia ya kukaa kwa muda mrefu katika mazingira na kuendelea kuleta athari tofauti ikiwepo athari kwa afya ya binadamu na mazingira zijulikanazo kama persistent organic pollutants (POPs), ambazo zilijulikana pia kama kemikali hatari kumi na mbili (dazani). Tatizo hili pia ni ghali kwa maana ya matibabu ya malaria na athari zitikanazo na matumizi ya kemikali hizo za sumu.

Kemikali zinazotumika pia katika kilimo kama za kuangamiza magugu na za kunyunyizia kuua mbu waenezao malaria zisipothibitiwa zinaathiri pia uoto wa asili ambao unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuondoa hewa ya ukaa (carbon dioxide) inayohusika na mabadiliko ya hali ya hewa. Pia zinaweza kuwa chanzo cha gesi ya metheni (methane) kutokana na mimea na wanyama wanaokufa na kuoza hivyo kuongeza mabadiliko ya hali ya hewa. Hii hutegemea ukubwa wa eneo zilikotumika.

Matumizi ya mafuta ya mitambo, uzalishaji umeme na vyombo vya usafiri, uharibifu wa misitu na matumizi ya kemikali katika kilimo ni kati ya shughuli zinazochangia mabadiliko ya hali ya hewa. Kama shughuli hizi hazitafanywa katika njia muafaka, zinaweza kuwa kikwazo cha jitihada na mikakati ya kupambana na umaskini katika nchi zinazoendelea, kama kufikia malengo ya MKUKUTA na pia Mipango ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).


Ili kupunguza tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa, gesi zote zinazohusika ni lazima zidhibitiwe na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa mapema iwezekanavyo. Hili linawezekana katika hatua tofauti ikiwepo ya mabadiliko ya sera za serikali na mashirika na pia mtu mmoja mmoja.

Hali hii ya mabadiliko inahitaji mchango wa kila mtu na dhamira ya kufanya mabadiliko. Ongezeko la joto na mabadiliko ya hali ya hewa kwa ujumla visitazamwe tena kama suala la kisiasa bali ni changamoto kubwa inayoikabili dunia yetu kwa sasa.
Kwa vile gesi zinazochangia ongezeko la joto katika kaya hutokana na uchomaji wa mafuta kwa ajili ya nishati kama kuzalishia umeme na kupikia (kuni, mkaa, mafuta ya taa) tunahitaji kutumia nishati kwa uangalifu zaidi kwa kutumia taa zinazotumia umeme kidogo, kuzima vifaa vya umeme pale tusipovihitaji, kutumia majiko banifu na kwa njia hii kwa ujumla wake itaweza kupunguza gesi hizo na pia kupunguza gharama za nishati.
Misitu inapoungua au kukatwa, kiasi kikubwa cha hewa ya ukaa inatoka na kuingia katika mazingira na ile iliyokuwa ikichukuliwa na misitu hiyo kukosa pa kwenda. Kwa hiyo ni muhimu sana kulinda na kuhifadhi misitu yetu, na kupanda miti mingi kabla ya kukata mmoja.
Matengenezo ya mara kwa mara ya magari na mashine zitumiazo mafuta kutasaidia kuongeza ufanisi katika matumizi ya mafuta na kupunguza matumizi na gharama. Tatizo la msongamano wa magari, na barabara mbovu linahitaji pia kushughulikiwa kwa mapana ili kupata ufumbuzi wa kudumu na pia kutahamasisha matumizi ya magari ya abiria hivyo kupunguza matumizi ya mafuta kwa ujumla.
Serikali izipitie na kurekebisha sera zake ili kutoa hamasa kwa uendelezaji wa nishati mbadala kama nishati ya jua, upepo na nyinginezo. Pia kuhamasisha jamii iweze kushiriki katika mipango endelevu ya kupambana na malaria na mbinu bora na endelevu za kilimo zisizotumia kemikali za sumu.


makala imeandaliwa kwa msaada wa shirika la maendeleo na Mazingira– AGENDA, lenye makao yake ofisi za Tanzania Bureau of Standards (TBS) Complex
,Ubungo Area P.O. Box 77266
Dar es Salaam, TANZANIA
Tel: +255 22 2450 213
Fax: +255 22 2450 836
E-mail: agenda@bol.co.tz
Website: www.agenda-tz.org

Labels:

1 Comments:

Anonymous Anonymous said...

Yes! Finally something about electronic music mastering.
My page: ozone 5 review

September 19, 2012 at 4:57 PM  

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA NDUGU

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home