Thursday, May 10, 2007

वाजसिलिमाली wanalia

DDC kupoteza mabilioni ya shilingi kwa miaka 7

Na Mobini Sarya

“SISI hatukatai kuboreshwa eneo hilo kama Shirika la Maendeleo Mkoa wa Dar es Salaam, (DDC) linavyotaka, tunachotaka baada ya eneo hilo kukamilika, watupangishe sisi wajasiliamali tuliovunjiwa vibanda vyetu” .

Hii ni kauli ya wafanyabiashara waliovunjiwa vibanda vyao eneo la DDC Kariakoo Dar es Salaam.

Wajasiriamali hao wameiomba Serikali,kuchunguza njia zilizotumika Kumpata Mkadarasi Mwekezaji anayetarajia kujenga vibanda eneo la DDC Kariakoo na wao kunyimwa tenda hiyo wakati walikuwa wanatoa pesa maradufu kuliko mwekezaji huyo.

Wajasiliamali hao wanasema hadi DDC kufikia uamuzi wa kuwavunjia vibada vyao na kumpa mwekezaji mwingine, walikwisha pitia ofisi mbalimbali za viongozi wa chama na Serikali.

Katika sakata hilo ambapo walalamikaji walikuwa wajasiriamali zaidi ya 40 waliokuwa na vibada eneo la ukumbi wa DDC Kariakoo wakipinga kuondolewa eneo hilo na kumpa mtu mwingine ili ajenge vibanda 52 na kuvipangisha kwa watu anaowataka hali iliyowalazimu kwenda mahakama kuu kitengo cha ardhi kufungua kesi wakipinga kupewa notisi ya kuhama ya siku 14, pili wakitaka wao wapewe tenda ya kuboresha eneo hilo na ikishindikana walipwe fidia ya kuhama .

Mahakama ilikubaliana na hilo pingamizi na kusema kuwa wapewe notisi kwa mjibu wa sheria na kuhusu kujenga eneo hilo waelewane nje ya mahakama ambapo walipelekwa mbele ya Jaji Kileo wa mahakama kuu kitengo cha ardhi,wakashindwa kuelewana.

Hatua iliyofikia hadi wao kupiga hodi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu (TAMISEMI), Mizengo Pinda.

Walifika TAMISEMI baada ya kuona maamuzi kutoka ofisi ya Rais kitengo cha Kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge wa Tanzania MKURABITA, yamepuuzwa.

Katika kikao cha MKURABITA, kilicho wakutanisha wajasiliamali na DDC, ilipendekezwa kuwa uongozi wa jiji uthibitishe kwamba wapangaji wa DDC Karikoo hawatafukuzwa hata baada ya maboresho kukamilika.

Pande zote mbili zilitakiwa ziandae mazungumzo nje ya Mahakama ili kuwezesha mazungumzo yaliyokwishaanza kuwa na maana, lakini pamoja na wajasiliamali hao kuondoa kesi mahakamani, DDC haikufanya nao mazungumzo.

Baada ya kufika kwa Pinda aliwashauri wajasiliamali hao kuchanga kiasi cha fedha za ujenzi hasa baada ya kubaini kuwa njia zilizotumika kumpata mkadandarasi, zinatia shaka, baada ya kuambiwa kuwa mkandarasi angetumia sh milioni 197 kujenga na kuendesha biashara kwa kwa miaka saba.

Kampuni inayodaiwa kuingia mkataba na DDC ni ya Nimeta Construction Ltd.

Mwanasheria wa Jiji, Paulo Mgasha alithibitisha kuwa mkataba huo ulifanyika mwaka 2004 baada ya kampuni nne kuwania tenda iliyotanganzwa na Bodi ya Wazabuni DDC, ambapo kampuni hiyo ilikidhi vigezo vilivyokuwa vinatakiwa .

Katika mkataba huo unaojulikana kama Build Oparate and Transfer (BOT), inaelezwa kuwa Nimeta walitakiwa wajenge vibanda 52 kwa gharama ya sh milioni 197 kwa kipindi hicho kisha wapangishe vibanda kwa kodi ya sh 300,000 kwa mwezi.

Chini ya mkataba huo, DDC italipwa sh milioni 50 kwa mwaka na mkataba huo ungedumu kwa miaka saba.

Mwanasheria wa jiji alisema kuwa pamoja na kuwa mkataba ni wa miaka saba lakini, DDC ingepokea malipo kwa miaka mitano na kumuachia Mzabuni miaka miwili akae bure bila kulipa kodi kama muda wa kuchuma faida yake.

Katika uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima kwa siku kadhaa sasa, umebaini kuwa viongozi wa wa chama na Serikali kila mmoja kwa nafasi yake wamejaribu kutengua maamuzi ya mkataba huo lakini mara zote DDC imekataa ingawa wakati DDC ikipokea milioni 50 kwa mwaka, mzabuni angevuna zaidi ya million 20 kwa mwezi.

Wajasiliamali hao wamesema ikiwa wataruhusiwa kuboresha eneo hilo kama DDC inavyotaka, watakuwa wanalipa zaidi ya sh milioni 200 kwa mwaka tofauti na sh milioni 50 zitakazolipwa na mkadarasi huyo.

“Wewe fikiria tulikubaliana kuwa ndani ya miaka saba atumie miaka mitano kurudisha hela yake ya ujenzi halafu huku akitulipa milioni 50 kwa Mwaka halafu akae miaka miwili bure leo ukimwambia avunje mkataba atakudai faida ambayo angeipata kwa miaka 2 , hao wajasilimali wanaweza kuzilipa?”alihoji mwanasheria

Lakini wajasilimali hao wanasema kuwa mzabauni atadaije hiyo faida ya miaka miwili wakati hajafanya kazi “MKURABITA wenyewe walituambia kuwa huu mkataba ukuvunjwa hauwezi kughalimu zaidi ya Milioni 4” wanasema wajasirimali hao

Katika uchunguzi huo wa Tanzania daima imebainika kwamba DDC iliingia mkataba na Kampuni ya Nimeta Consruction, mwaka juzi kwa maelewano kwamba atavunja vibanda vyote 40 vinavyozunguka ukumbi wa DDC Kariakoo kisha atajenga vibada vipya 52 kwa Gharama ya shingi Milion 197 na atakaa eneo hilo kwa mjibu wa mkataba wa BOT ‘Build Oparate and Transfer’ kwa muda wa miaka saba.

Jambo hilo limewashitua wajasilimali hao ambao tayari wamekwisha changa shilingi milioni 200 ya kujenga eneo hilo zaidi ya shilingi 197 ambazo mwekezaji atatumia , lakini wamenyimwa nakuambiwa waondoke jambo ambalo wanaomba Serikali kuingilia kati na kuchunguza mkataba huo unaolitia aibu Taifa.

Malalamiko ya wajasiriamali hao yanadaiwa kumfikia Waziri mkuu Edward Lowassa, akaagiza vibanda visivunjwe lakini agizo lake likacheleweshwa TAMISEMI.

Katika uchungunzi huo imebainika kwamba tayari DDC wamekwisha chukua shilingi milioni 4.16 kama malipo ya awali ya mkataba kutoka kwa Nimeta, wakati wafanyabiashara wanaoondolewa eneo hilo wako tayari kulijenga kama inavyotakiwa kwa gharama zao bila riba kisha kulipa kodi milioni zaidi 20 kwa mwezi yaani vibanda 52 kwa shilingi laki 5 kwa kila kimoja.

“sisi hatukatai maboresho hayo yanayotakiwa tunachosema kuwa yule mkandarasi ajenge tu nakuondoka kama alivyopendekeza Mkuu wa Mkoa Abbas Kandoro, sio tena kuendesha huku akipangisha watu anaowajua sisi tunafukuzwa tuende wapi, kwanini gharama za ujenzi tusilipie ili tubaki wao wanataka kutuondoa”?alisema mmoja wa wajasiliamali hao.

Wafanyabiashara hao wanadai kuwa njia zilizotumika kumpata huyo mwekezaji hadi wao kuondolewa ni chafu , kwani haiwezikani shirika likatae kuchukua shilingi milioni 200 kwa mwaka baadala yake likubali shilingi milioni 50 , hali inayoonyesha kuwa ndani ya Mwaka mmoja zitakuwa zinavunwa zaidi ya shilingi mil 400 ambapo kwa miaka saba zitavunwa karibu bilioni 2.

Kutoka na hali hiyo wajasiliamali hao wameiambia Tanzania Daima kuwa ikiwa itashindikana kupewa nafasi ya kujenga wanaomba utengenezwe utaratibu maalum kama maboresho yakikamilika waruhusiwe kurudishwa katika maeneo yao ya awali bila kuzuiliwa kwani ndipo wanapatia riziki.

“Huu mkataba ni mnono kila mmoja aliyeshiriki hapa amejua alichopata na mwekezaji anajaribu kufanya kila awezalo kuona anafanikiwa, mkataba unazungumzia mamilioni lakini ukiangalia jumla ya vibada 52 kwa mwezi atapata karibu mil 312 kwa mwaka na mara miaka saba utaona mwenywe kuwa ni aibu jiji DDC kuambulia million 50 kwa mwaka tena mitano” kilisema chanzo kimoja.

Mgasha aliliambia Tanzania Daima kuwa wakati wanakubaliana na huyo Mwekezaji kutumia shiligi milioni 197 vifaa vya ujenzi vilikuwa bei chini lakini kwa sasa itabidi zitumike kama shilingi milioni 400 hivyo kumruhusu kupandisha kodi kama kama atakavyoona.
Baada ya Pinda kusikiliza malalamiko ya wajasilimali hao aligundua kuwa mkataba huo ulikuwa umegubikwa na uozo akaamua kuitisha kikao cha viongozi wa serikali mkoa wa Dar es Salaam na Manispaa ya Ilala kisha akaunda tume ya watu nane chini ya Wilson Mukama ambaye ni naibu Katibu Mkuu TAMISEMI.

“Baada ya kupata maelezo kutoka pande zote zinazohusika na mgogoro huu nimeridhika kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi na masharti ya mkandarasi huyo kuhusiana na ujenzi na utumiaji wa majengo hayo baada ya kukarabatiwa yana utata na kwamba mustakabari wa wapangaji uliopo sasa haujulikani”

Kutokana na utata huo nimeunda tume itakayochunguza mazingira na mchakato wa kumapata mkadarasi huyo na kupendekeza na kupendekeza hatua muafaka za kuchukua kumaliza mgogoro huu” ilisema sehemu ya barua kwenda kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa wa Dar es Salaam,Yusufu Makamba 12 Mei 2006.

Hata hivyo tangu tume hiyo iundwe nakupewa rejea nane ikiwamo ya kuchunguza njia zilizotumika kumpata Mkandarasi huyo haikuwahi kufanya kazi zake ,

baadala yake katika mazingira ya kushangaza Mkama aliamuandikia Meneja wa DDC, Mhando Muya Disemba 29 mwaka 2006 akimweleza kuwa wizara imebaini kuwa utekelezaji wa magizo yake iliyotoa 11 Mei 2006 yanaweza kupelekea mgogoro wa kisheria, kwani maamuzi yake yatakuwa yanakiuka maamuzi ya Mahakama ambayo yaliruhusu kuendelea kwa ujenzi.

Hata hivyo Mkama hakueleza wazi ni lini na katika kesi gani Mahakama iliamua kuwa ujenzi uendelee wakati wajasialimali walikuwa wamesha ondoa kesi ya Msingi Mahakamani, jambo ambalo wajasiliamali hao wanaona kama wanasalitiwa kwani hata huyo Mukama wanasema awali alikuwa Jiji kwa hiyo huenda alihusika kufanikisha hiyo tenda.

Baada ya Muya kupata taarifa hiyo aliwapa wajasilimali notisi ya mwezi mmoja jambo lililosababisha wakimbilie kwa Rashid Kawawa ambaye alimwagiza katibu Mkuu wa CCM alishughulikie kichama, naye alimwagiza Msaidizi wake Capt. Ligola.

ambapo viongozi wa chama na serikali walikutana kisha wakaita pande zote machi 7 Mwaka huu kwa mkuu wa mkoa Abbas Kandoro ambaye aliwaambia DDC kuwa wabadilishe masharti ya mkataba, mkandarasi ajenge tu na kulipwa kisha aondoke awachie wale wajasiliamali jambo ambalo DDC walipingana nalo.

Nakuamua kutoa notisi ya mwezi mmoja machi 30 mwaka huu ambapo Mei 3 walikwenda kuwavunjia vibada vile tayari kwa kumpa huyo mkandarasi mwekezaji, bila wajasilimali hao kujua mastakabali wao, huku wakiomba kurudishwa kwenye eneo hilo baada ya maboresho kukamilika, ingawa wamesema kwa akipindi chote cha Miaka 7 DDC itapoteza mabilioni ya shilingi na kuambulia million 250 tu.

“Hili shirika litakufa we fikiria kama yule mkandandarasi atakuwa anapangisha kwa gharama kati ya laki tano hadi nane ambapo atakuwa anavuna zaidi ya shilingi milioni 25 kwa mwezi. Katika muda wa miaka saba atakuwa amepata kiasi gani?”,alihoji mmoja kati ya wajasiliamali hao.

www.mobinday.blogspot.com .0753 399 579 mobinsons@yahoo.com.
.

Labels:

0 Comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA NDUGU

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home