Thursday, April 26, 2007

सेरिकाली इमेज़ामिलिया kuuwa watu वाके?

HIVI KARIBUNI SHIRIKA MOJA LINALOPA HUSIKA NA MASUALA YA KIJAMII, KWA KUSIMAMIA MAENDELEO NA KUTUNZA MAZINGIRA LILITUMIA SIKU YA MALARIA KUONYA HATARI INAYOTUKABILI TANZANIA KAMA TUTATUMIA DAWA YA DDT KUPAMBANA NA UGONJWA HUO.
AGENDA FOR ENVIRONMENT AND RESPONSIBLE DEVELOPMENT

SIKU HUYO HIYO WAZIRI WA AFYA AKIWA MKOANI KAGERA ALIWAMBIA WANANCHI KUWA DAWA HIYO ITAANZA KUTOLEWA BURE KWA MWANANCHI ATAKAYEHITAJI.

SASA NI BORA KILA MMOJA ASOME HAYA AJIDHIHIRESHE MWENYEWE KAMA NI BORA KUITUMIA AU NI KYAMA KINAKUJA FUATANA NA MWANDISHI WETU MOBINI SARYA UFAHAMU YALITOJIRI HUKO KWENYE MKUTANO HUO

MAADHIMISHO YA SIKU YA MALARIA AFRIKA TAREHE 25 APRILI 2007


Malaria ni nini?
Malaria ni ugonjwa unaotishia maisha unaoenezwa na mbu kwa njia ya vijidudu (parasite) vijulikanavyo kama plasmodium ambavyo vinaenezwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu jike aina ya anofelesi (anopheles). Mbu aina hii hutumia damu kwa ajili kukuzia mayai yake.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa kuwa 40% ya watu duniani hasa kutoka nchi maskini zaidi wapo katika hatari ya kuambukizwa malaria. Ugonjwa wa malaria unawapata watu zaidi ya milioni 300 na wastani wa vifo milioni moja kila mwaka.
Kiasi cha 80% kati ya vifo vyote vya malaria hutokea barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara , na wengi wao wakiwa ni watoto chini ya umri wa miaka mitano. Wanawake wajawazito na watoto ambao bado hawajazaliwa wapo pia katika hatari kubwa kuambukizwa ugonjwa wa malaria, ambao ni chanzo kikubwa cha kuharibika kwa mimba, kuzaliwa na uzito mdogo na upungufu wa damu kwa wazazi.
Malaria huenezwaje?
Vijidudu vya malaria (parasite) huingia katika mwili wa binadamu wakati mbu jike aina ya anofelesi (anopheles) mwenye vijidudu hivyo anapomnyonya damu. Katika mwili wa binadamu vijidudu hivyo hubadikilika badilika kwa namna tofauti. Katika hatua tofauti, hushambulia mfumo wa kinga ya mwili, kuathiri ini na chembe chembe nyekundu za damu. Baadaye hubadilika katika namna ya kumwathiri tena mbu wakati anapomuuma binadamu aliyekwisha shambuliwa. Ndani ya mwili wa binadamu vijidudu hivyo hukomaa na kufikia hatua ya kuweza kumdhuru tena binadamu wakati atakapoumwa tena na mbu baadaye, kati ya siku 10 na 14 au zaidi.
Dalili za ugonjwa wa malaria huanza kuonekana kati ya siku 9 na 14 baada ya kuumwa na mbu mwenye vijidudu vya malaria, ingawaje hutofautiana kwa aina ya vijidudu (plasmodium species). Malaria husababisha homa, kuumwa kichwa, kutapika dalili nyinginezo kama mafua. Malaria inaua kwa kuzishambulia na kuharibu chembe chembe nyekundu za damu na kusababisha upungufu wa damu kwa kuziba mishipa inayobeba damu. Hali hii husababisha kuathirika kwa ubongo (cerebral malaria) na viungo vingine muhimu. Kiasi kikubwa cha malaria barani Afrika husababishwa na vijidudu hatari aina ya Plasmodium falciparum.
Malaria, pamoja na UKIMWI (HIV/AIDS) na kifua kikuu (TB), ni maadui wakubwa kwa afya ya jamii na changamoto ya maendeleo ya kiuchumi hasa barani Afrika. Malaria inakadiriwa kuligharimu bara la Afrika kiasi cha zaidi ya dola za Marekani (US$) bilioni 12 kwa mwaka na kupungua kwa pato la taifa.
Sababu za kuongezeka malaria barani Afrika
Sababu za kuongezeka kwa malaria barani Afrika ni pamoja na sababu za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa vinavyosababisha kuenea kwa malaria mfano ongezeko la joto (global warming), kuongezeka kwa usugu vijidudu vya malaria na mbu kwa dawa zinazotumika na shughuli au kuhama kwa binadamu. Vile vile, nchi nyingi barani Afrika hazina miundombinu na rasilimali muhimu kwa mapambano endelevu dhidi ya malaria.
Hali ya malaria nchini Tanzania
Kulingana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, taarifa ya mwaka 2002/2003 inaonesha kuwa wastani wa watu 100,000 nchini hufa kwa malaria kila mwaka. Ugonjwa huu ni hatari kwa afya na una athari kubwa kiuchumi. Kwa mfano, mwaka 2003 malaria iliigharimu Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 120 (dola za Marekani (USD) 120 milioni) kwa ajili ya gharama za matibabu na muda wa kazi uliopetea kwa wagonjwa kwa mwaka.
Kujikinga na malaria na matibabu yake
Vijidudu vya malaria vimejenga usugu wa dawa moja hadi nyingine na viutalifu (kemikali) vya kuulia mbu waenezao malaria. Baada ya miaka kadhaa ya utafiti wa chanjo bado haujaleta matunda yaliyokusudiwa. Bado sayansi haijatoa majibu ya “risasi thabiti” dhidi ya malaria haitarajiwi itapatikana dawa moja na pekee kwa tatizo hili.
Kuwakinga akina mama wajawazito dhidi ya malaria kwa mfano kutumia njia mbadala na tofauti, nyavu za mbu (neti) zilizotiwa kemikali-dawa (ITNs), kuboresha afya ya akina mama wajawazito na wazazi, kupunguza maambukizo na vifo vya watoto wachanga. Njia za haraka za matibabu kwa kutumia dawa madhubuti kama mchanganyiko wa atemisinini (artemisinin-based combination therapies - ACTs), vitaokoa maisha ya wengi. Nchi za Afrika zikitekeleza njia hizi kwa upana na kufuatilia utekelezaji wake tatizo la malaria litapungua.
Changamoto kubwa inayoikabili Africa katika kupambana na malaria ni usugu wa dawa zilizotumika au zinazoendelea kutumika. Usugu wa dawa rahisi na zilizotumika zaidi umeonekana kote barani Afrika. Matokeo ya usugu huo ni nchi nyingi kubadili sera za matibabu na kutumia dawa ambazo ni ghali zaidi na pia mchanganyiko wa dawa ambao unatarajiwa utapunguza usugu huo.
Siku ya malaria Afrika
Siku ya malaria Afrika huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Aprili baada ya Mkutano wa kwanza nchi za Afrika kuhusu malaria uliofanyika Abuja, Nigeria tarehe 25 Aprili 2000 ambapo viongozi wa nchi 44 zinazoathiriwa zaidi na malaria walisaini Azimio la Abuja. Azimio hilo ni ahadi za serikali za nchi hizo kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza maambukizo na vifo vitokanavyo na malaria kwa nusu ifikapo mwaka 2010, kipindi cha malengo ya mpito mwaka 2005, na kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia yanayohusiana na malaria. Lengo la 1: Kuondoa umaskini uliokithiri na njaa, na Lengo la 6: Kupambana na UKIMWI (HIV/AIDS), malaria na magonjwa mengine – kumaliza na kuanza kubadili milipuko ya malaria na magonjwa mengine makubwa.

Siku ya malaria Afrika mwaka 2006 ilikuwa na ujumbe “Upatikanaji wa Matibabu Thabiti ya Malaria ni Haki ya Binadamu.” Kauli mbiu ya siku ya malaria mwaka huu (2007) ni “Ondoa Malaria Afrika Sasa” na ujumbe “Uongozi na Ushirikiano kwa Matokeo" na unaonesha ni kwa njia gani tunahitaji kuiondoa Afrika katika janga la malaria. Unasisitiza uongozi imara na ushirikiano thabiti kama njia mahsusi kufikia malengo la kuondoa malaria na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kupambana na malaria na kuelezea jukumu la kimataifa na rasilimali za kupamabana na malaria.
Kumekuwa na maendeleo yenye matumaini baada ya Azimio la Abuja mwaka 2000. Kwa takribani nchi 20 za Afrika zimepunguza au kuondoa kabisa kodi na ushuru wa vyandarua vilivyotiwa kemikali-dawa (ITNs) kuzifanya ziweze kununuliwa na watu wa kipato cha chini. Jitihada hizo zinajumuisha upatikanaji wa matibabu kwa wakati, kusisitiza matumizi ya vyandarua vilivyotiwa kemikali-dawa, uimarishaji wa mbinu za kupambana na wadudu waenezao magonjwa. Pia kuwakinga akina mama wajawazito na malaria na kupambana na milipuko ya malaria.
Njia za kujikinga

Kumekuwepo na njia tofauti za kujikinga na malaria zinazopendekezwa na wadau tofauti katika kupambana na malaria, afya na mazingira. Mwezi Septemba 2006, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) lilitangaza kuunga mkono matumizi ya kemikali aina ya DDT kunyunyiziwa ndani ya nyumba (DDT - Dichloro-dipheny-trichloroethane) kama njia ya kupambana na malaria. Kufuatia tangazo hilo , Tanzania imeonesha nia yake ya kuanza kutumia tena DDT ambayo ilishapigwa marufuku kwa ajili ya kupambana na malaria.

Inaelezwa kwa urahisi kuwa kutumia DDT kutaokoa maisha ya maelfu ya watu wanaokufa kwa malaria duniani lakini ni muhimu pia kukumbuka madhara yake ya muda mrefu kwa afya na mazingira. Mkataba wa Kimataifa wa Stockholm kuhusu kemikali zinazodumu na kuleta athari kwa afya na mazingira kwa muda mrefu baada ya kutumika (Persistent Organic Persistent - POPs) ulishaiorodhesha DDT kama moja ya kemikali zinazotakiwa kuondolewa katika uzalishaji na matumizi. Tanzania imeridhia Mkataba huo ambao ulisainiwa mwezi Mei 2001 na kuanza kutumika kisheria mwezi Mei 2004.

Ingawaje Mkataba unatoa ruhusa ya kutumia DDT kwa ruhusa maalum, kuanza kuitangaza kwa matumizi katika nchi zilizoathirika na malaria kunaenda kinyume na malengo ya Mkataba wa Stockholm ambayo ni kukinga afya ya binadamu na kemikali za aina hiyo (POPs).

POPs kwa ujumla ni kemikali zinazodumu kwa muda mrefu katika mazingira baada ya kutumiwa, zikisambaa sehemu tofauti kwanjia ya maji na hewa na kujikusanya katika sehemu zenye mafuta za miili ya viumbe hai. Kemikali hizi zina tabia ya kuongezeka kiwango chake kutoka ngazi moja hadi nyingine katika mfumo wa chakula, mfano kiwango kilichopo katika samaki huongezeka katika mwili wa binadamu atakeyemla. Pia huingia katika miili ya watoto wachanga kutoka kwa mama wakati wa kutunga mimba. Kwa kifupi kemikali hizi ni sumu kwa viumbe na mazingira na kwa tabia yake huendelea kuathiri kizazi kimoja baada ya kingine muda mrefu baada ya kutumika.

Muhimu zaidi ni kuwa Mkataba huo unahamasisha fedha zinazohitajika kwa ajili ya kujikinga na kudhibiti malaria, ukisisistiza njia mbadala, salama, madhubuti na mikakati ambayo haitakuwa tena na madhara kwa afya ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Utafiti uliofanywa umeonesha kwamba kemikali za POPs zinapoingia katika mwili wa binadamu huchangia kuongezeka kwa magonjwa ya saratani (kansa), kuharibu uwiano wa vichocheo vya mwili (hormones) katika mwili, kuathiri mifumo ya fahamu, nguvu za uzazi na uwezo wa kuzaa (utasa), kuongeza matatizo ya kisukari, kupunguza kinga ya mwili dhidi ya magonjwa. Kemikali hizi pia huingilia mfumo wa ukuaji na uelewa kwa watoto wadogo.

Huko Marekani kwenyewe na penginepo duniani DDT inaaminiwa kuwa chanzo cha saratani (kansa). Pia matatizo ya uzazi yanayohusiana na DDT yamefanyiwa utafiti kwa wanyama na kuonesha kuchangia kupungua kwa nguvu za uzazi na utasa. Hii inamaanisha kwamba madhara hayo yanatokea kwa binadamu pia kuzingatia tabia ya DDT kama POPs nyingine ya kudumu kwa muda mrefu katika mazingira, kujikusanya na kuongezeka kiwango katika ngazi za mfumo wa chakula. Utafiti wa karibuni umeonesha madhara ya mfumo wa fahamu ikiwa ni pamoja na kuchelewa kukua kwa watoto wachanga walioathiwa na DDT

Utafiti pia umeonesha athari katika kupungua kwa kiwango cha maziwa ya mama wakati wa kunyonyesha. Watafiti wa Marekani wameeleza kuwa kemikali inayotokana na kuvunjika kwa DDT inayojulikana kama DDE, inaweza kuchangia kuzaliwa kwa watoto kabla ya wakati na kuzaliwa wakiwa na uzito mdogo. DDT na kemikali zinazotokana na kuvunjika kwake zimeonekana pia katika damu na maziwa ya binadamu katika tafiti nyingi zilizofanyika sehemu mbalimbali duniani.

Tatizo lililosababisha DDT kushindwa kuua mbu waenezao malaria ni mbu hao kujenga usugu. Usugu wa mbu kwa kemikali hizo ulianza kuonekana Afrika mwanzoni na katikati ya miaka ya 1955, na kufikia mwaka 1972 aina 19 za mbu duniani walikuwa wamejenga usugu kwa DDT.

Utafiti wa karibuni waoanisha DDT na kupungua kwa nguvu za uzazi kwa wanaume

Hivi karibuni watafiti wa masuala ya utabibu nchini Afrika Kusini walithibitisha kuwepo kwa tatizo kubwa la kupungua kwa kiwango cha mbegu za kiume na uharibifu wa mfumo wa uzazi kwa wanaume unaooanishwa na matumizi ya DDT katika kampeni dhidi ya malaria.

Utafiti huo ulioshirikisha zaidi ya vijana wa kiume 300 katika Jimbo la Limpopo, pia umeonesha hatari iliyopo kwa afya ya uzazi ya wanaume wanaoishi maeneo ya vijijini katika majimbo ya KwaZulu-Natal na Mpumalanga ambapo DDT inaendelea kutumika. Taarifa ya utafiti huo uliochapishwa katika jarida la kimataifa la taarifa za utafiti, lijulikanalo kama Journal of Andrology, ni kati ya tafiti kubwa nchini humo juu ya madhara ya DDT.

Profesa Tiaan de Jager, aliyekuwa kiongozi wa utafiti huo alitoa taarifa katika gazeti la The Mercury on Wednesday kuwa sasa kuna uthibitisho dhahiri kwa Idara ya Afya kuzingatia athari za kiafya zitokanazo na matumizi ya DDT, na kufikiria kutafuta njia mbadala na salama za kupambana na malaria. 'Kuna madhara ya moja kwa moja yatokanayo na DDT, na kiasi kikubwa cha DDE ambayo ni matokeo ya kuvunjika kwa DDT kinaonesha matatizo ya kiafya ya muda mrefu'
De Jager na watafiti wenzake kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Utabibu cha Pretoria, (University of Pretoria School of Health Systems and Public Health), waligundua "kiasi kikubwa sana" cha DDT na DDE katika damu iliyochukuliwa kutoka kwa wanaume jimboni Limpopo katika miaka miwili ya utafiti huo ambao bado unaendelea.

Watafiti hao pia wanasema walipima sampuli kutoka kwa wanaume 311 wa kati ya umri wa miaka 18 na 40 katika maeneo ya Thoyohandou na Vhembe huko Limpopo . Uchunguzi wa maabara wa sampuli hizo ulionesha kiasi kikubwa cha kupungua kwa kiwango cha mbegu za kiume, kasi ndogo ya mbegu na kupungua kwa uwezo wake kuelekea kurutubisha yai la kike kwa ajili ya kupata watoto. Watafiti hao wanasema kuna uthibitisho dhahiri kutoka duniani kote ambapo DDT imesababisha mabadiliko ya homoni na mlingano wake katika mwili (endocrine-disrupting and altering the normal human hormone balance), na kuingilia mifumo na viungo vya uzazi. Utafiti huo pia umeonesha uhusiano wa wazi kwa kuwepo viwango vikubwa vya DDT kwa watu ambao nyumba zao zilinyunyiziwa DDT kujikinga na malaria.

Taarifa hiyo imehitimisha kuwa uwezo wa kuzaa kwa wanaume waliopo katika eneo hilo ambapo DDT imetumika huko Limpopo utakuwa umeathirika. Kwa mfano, asilimia 28 ya wanaume walikuwa na upungufu wa mbegu za kiume, asilimia 99 walikuwa na mbegu zilizobadilika maumbile na ukubwa, na asilimia 32 walikuwa na mbegu ambazo uwezo na kasi yake ya kupenya umepungua. Matokeo haya siyo tu kwamba yanawahusu wakazi wa Limpopo bali pia maeneo yote duniani ambapo DDT imenyunyiziwa au itanyunyiziwa. Kuna haja ya kuelekeza nguvu zaidi katika kutafuta, kutumia na kuendeleza njia mbadala na salama kwa afya na mazingira katika kukabiliana na tatizo hili.

Njia mbadala

Ni rahisi kufikiria kunyunyiza DDT ndani ya nyumba nchini Tanzania lakini ni lazima ikumbukwe kuwa tunao udhaifu wa kutekeleza mipango mbalimbali ya kitaifa zikiwepo sera na sheria. Mapungufu haya yanaweza kusababisha DDT hiyo ikaingia katika kilimo na hivyo kuzidi kudhuru afya za watu na kuharibu soko la bidhaa za kilimo hivyo kuongeza umaskini.


Programu mchanganyiko kwa kushirikisha jamii ni njia muafaka ya kujikinga na malaria. Hii haimaanishi kubadili kemikali moja kwa nyingine, bali kujenga mkakati madhubuti ambao unaweza kuhusisha:
a) kutambua mapema dalili za malaria na kupata tiba mapema;
b) ushirikishwaji wa jamii katika kutoa taarifa za mlipuko wa malaria na usafi wa sehemu zote ambazo ni vyanzo na mazalia ya mbu; na
c) kupunguza kabisa matumizi ya kemikali za sumu kwa kutumia kemikali zitokanazo na mimea kama pareto (pyrethroid).

Programu nyingine zinaweza kuhusisha jitihada za kupunguza mazalia ya mbu kwa kuondoa makusanyiko ya maji na kujenga nyumba zenye kupunguza uwezekano wa mbu kuingia ndani (vizuizi vya mbu).



Mapendekezo

1. Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea hasa Afrika zinahitaji msaada katika kutafuta mbadala thabiti na wa kudumu na siyo kurejesha matumizi ya DDT;
2. Kwa dhamira ya kweli ya kupambana na malaria, serikali zinahitaji kutekeleza ahadi zake katika Azimio la Abuja na kuongeza bajeti za afya kwa ajili ya mipango na programu za muda mrefu;
3. Kuna haja ya kuwa na njia za uhakika na za kudumu za fedha inayolenga kusaidia mikakati katika ngazi ya jumuiya za kiraia na jamii kwa ujumla ikihusisha uimarishaji wa mifumo ya ujenzi, usafi wa mazingira na sera za uhakika za kupambana na umaskini;
4. DDT siyo “risasi rahisi” inapochukuliwa kwa ujumla katika madhara kiafya na kimazingira hivyo njia muafaka zaidi itakayookoa maisha ya wengi kwa muda mrefu inahitajika ikihusisha dhamira ya kweli na shirikishi;
5. Zinahitajika sera za wazi juu ya DDT na mwongozo unaolenga kutekeleza matakwa ya Mkataba wa Stockholm kwa nchi zote zilizouridhia;
6. Nchi zilizoendelea na mashirika mengine kusaidia Afrika katika kupata na kuendeleza suluhisho muafaka na endelevu la tatizo la malaria.

Kwa uongozi madhubuti na ushirikiano, kwa pamoja tutapata suluhisho muafaka juu ya tatizo la malaria barani Afrika!

Mwenyekiti Mtendaji

r

0 Comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA NDUGU

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home