Wednesday, August 1, 2007

* Dunia itatikisika, binadamu atasaga meno

Mwisho wa dunia umefika!

* Ishara za manabii zaelekea kutimia

* Uchafuzi wa mazingira nalo ni tatizo

Na Musa Ngarango

MENGI yamesemwa na yanaendelea kusemwa kuhusu tukio la kutisha la siku yenye utata ya kutoweka kwa dunia hii tunamoishi.
Je, ni kweli dunia hii kuna siku itafikia tamati? Misingi yake itavunjwa na tawala za kibinadamu nazo kuangamizwa kabisa?
Bila shaka hayo ni maswali yenye kukanganya sana ambayo kila anayeulizwa hutoa majibu tofauti. Wapo wanaosema dunia hii haina mwisho, ila mwisho ni pale binadamu anapofikwa na mauti, lakini si suala la dunia nzima.
Katika hilo, wanazuoni wa masuala ya kidini wanaikosoa sana dhana hiyo na kwenda mbali zaidi kwa kuiita dhana ya kishetani. Wanazuoni hao wanabainisha na kusema kwamba dunia hii ni lazima ifikie tamati (kiama) ambapo siku hiyo kila binadamu atalipwa kulingana na matendo yake.
“Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shamba asilejee nyuma.” Luka 17: 31. “Na atasema mwanadamu (wakati huo): Oh! Ina nini (leo hii ardhi)?” Qur’aan 99:3 Suratuz zilzal.
Aya hizi zinazopatikana katika vitabu vitakatifu vya imani, Biblia na Kurani, ni miongoni mwa aya ambazo zimebashiri mwisho wa dunia na mara kwa mara hutumiwa na wanazuoni wa kidini kuwa mifano.

Tuitazame dunia na sayari nyingine

Ukiondoa sayari ya Pluto iliyogunduliwa mwaka 1930 na mwanaanga kutoka Marekani, Clyde Tombaugh, ambayo hata hivyo iliondolewa katika mlolongo wa sayari kwa kupigiwa kura na wanasayansi waliokutana mjini Prague, Jamhuri ya Czech mwaka 2006, dunia imebaki kuwa miongoni mwa sayari nane ambazo ni Mercury, Venus, Jupiter, Mars, Saturn, Uranus na Neptune.
Katika mlolongo wa sayari, dunia ni sayari ya tatu kutoka lilipo jua ukiachilia mbali Mercury na Venus, pia ni sayari ya tano kwa ukubwa miongoni mwa sayari zote.
Wanasayansi katika utafiti wao ambao unadaiwa kufanyika miaka ya 1800 hadi 1900 kabla ya Kristo, walibaini kwamba dunia tunayoishi na sayari nyingine zinazolizunguka jua zilikuwa kitu kimoja.
Wanasayansi wanadai kwamba mwanzo wa dunia ulipatikana kwa zaidi ya miaka bilioni tano ambapo mchanganyiko wa madini, gesi na vumbi ulifanya aina fulani ya moshi uliojizungusha kwa kasi ya ajabu kwa muda wa miaka hiyo.
Ingawaje wanasayansi hawabainishi wazi kwamba vitu hivyo yaani madini, gesi na vumbi, vilitokea wapi, wanaendelea kusema kwamba kutokana na kasi hiyo ya kujizungusha, palizuka joto ambalo hatimaye lilisababisha mapande makubwa yaliyosambaratika angani na mapande hayo ndizo hizi sayari, yaani ‘Solar System’ kwa lugha ya kitaalamu.
Dunia, inakadiriwa kuwa na ukubwa wa zaidi ya maili milioni mia tano na kipenyo cha kilometa elfu 12.8
Sayari hiyo inazunguka katika njia yake kwa kasi, inatembea maili 70,000 kwa saa moja, mwendo huo kimahesabu ni sawa na wastani wa maili 1,166 kwa muda wa dakika moja, dunia hukimbia umbali wa maili 19.

Tabaka za ajabu

Wanasayansi wanasema kwamba dunia hii ina tabaka kwazo, kila moja ina umuhimu katika maisha ya binadamu. Wanabainisha tabaka hizo zipo saba ambazo ni Troposphere, Stratosphere, Ionosphere Thermosphere, Ozone layer, Exosphere na Mesosphere.
Katika makala hii nitazielezea baadhi ya tabaka hizo kwa sababu inabainishwa kwamba kila moja inatenda kazi yake katika hali ya kushangaza sana.

Troposphere: Tabaka hili lililobeba kiwango kikubwa cha aina zote za hewa zinazokadiriwa kufikia zaidi ya asilimia 90 liko umbali wa maili 13 kutoka usawa wa ardhi, limebeba asilimia 78 ya hewa ya Nitrogen ambayo husaidia kuzuia baadhi ya sehemu za dunia zisigande unapofika wakati wa usiku ambapo miale ya jua huakisi upande wa pili na kuufanya upande mwingine kukosa joto.
Stratosphere: Tabaka hili ni tofauti na tabaka la awali, lenyewe lina hali nzito ya hewa na hali hiyo huzidi kupanda kadiri unavyoelekea angani. Tabaka hili ndipo kunapopatikana njia za kitaifa na kimataifa za usafiri wote wa wa vyombo vya anga.
Ionosphere: Tabaka hili ndilo lenye hali ya umeme ambayo hutokana kwa nguvu fulani zitokanazo na jua, nguvu hizo zenye mifumo ya kiumeme husaidia utawanyaji wa mawasiliano kupitia satellite za redio, televisheni au mitandao ya simu.
Tabaka hilo ndilo husaidia sauti za vituo vya redio au televisheni kusikika hewani, kwani sauti au picha inaponaswa katika satellite ya angani, nayo hufanya kazi ya utawanyaji katika tabaka hilo.
Kama hiyo haitoshi, katika tabaka hilo ndipo inapopatikana mifumo ya radi ambayo hufanya kazi ya kuyatandaza mawimbi ya kiumeme yanayorundikana na inapotokea hali hiyo, ndipo hata mifumo ya kidunia ya mawasiliano ya redio au televisheni hutetema kwa hali ya mikwaruzo.
Ozone Layer: Tabaka hili ndilo kiungo kati ya miale ya jua na dunia. Hufanya kazi ya kuchuja miale ya jua isiakisi moja kwa moja duniani miale ambayo kama inaruhusiwa iifikie dunia moja kwa moja, itafuta kabisa mifumo ya maisha ya viumbe hai.
Kiwango kikubwa cha miale ya jua kinachohifadhiwa katika tabaka hili, kiasi chake kidogo hubadilishwa na kuwa mifumo umeme ambao ndio hutumika katika tabaka la Ionosphere.
Pia tabaka hilo huifadhi kiwango kikubwa cha hewa chafu ya Carbon dioxide ambayo huzalishwa na binadamu kwa kupumua, mifumo ya sumu itokanayo na silaha, uchafuzi wa mazingira ukiwemo wa moshi mzito utokanao na shughuli za viwanda.
Kama hiyo haitoshi, tabaka hilo pia huzuia mawe yanayotoka katika sayari nyingine yasiifike dunia ambapo mawe hayo husukumwa na upepo mkali unaorindima katika sayari hiyo kisha huunguzwa na moto mkali uliopo eneo hilo ambapo hatimaye hubakia vipande vidogo vya chuma vinavyoanguka kuelekea ardhini.

Dunia kutoweka hivi

Inaonywa kwamba kutoweka kwa dunia kutatokana na hali mbaya ya uchakavu wa tabaka la Ozone linaloendelea kuchakaa kadiri dunia inavyozidi kuzeeka na kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira.
Kama nilivyoeleza awali, kwamba miongoni mwa kazi za tabaka hilo ni kuhifadhi ziada ya hewa chafu inayotoka duniani katika hali mbalimbali kama vile, moshi wa magari, na ule utakao viwandani, kemikali za sumu zinazotoka katika vifaa vya kivita kama vile makombora ya nyuklia na kadhalika.
Inatanabaishwa kwamba kutokana na hali mbaya ya uzalishaji mkubwa wa hali ya hewa chafu unaosambaa duniani na kusafiri mpaka kwenye tabaka hilo shupavu, imefika wakati limeanza kuchakaa.
Hali hiyo mbaya ya uchafuzi wa mazingira ambayo kila kukicha imeendelea kushamiri kwa kasi ya ajabu, italifanya tabaka hilo kushindwa kuhimili na hivyo kuanza kuvujisha mionzi hatari ya jua na kuiruhusu kufika moja kwa moja duniani.
Hali hiyo itasababisha ongezeko la joto duniani na hata kuleta magonjwa ya saratni ya ngozi na damu na kusababisha kupunguza siku za kuishi kwa viumbe hai.
Wanasayansi wanaonya kwamba kama hali ya uchafuzi wa mazingira itaachwa iendelee, italifanya tabaka la Ozone kuharibika kabisa na hapo ndipo tamati ya maisha ya viumbe hai itakapowadia.
Inasemekana kwamba hewa chafu (carbon dioxed) inayohifadhiwa katika tabaka hilo, nayo itapoteza mwelekeo, hali itakayosababisha hewa hiyo kufumuka na kushuka duniani kwa kasi ya ajabu na hatimaye kusambaa baharini na nchi kavu.
Hali hiyo yenye kuogofya itakapojiri, itaharibu mifumo ya anga inayosababisha mvua kunyesha na kwa mantiki hiyo unyeshaji wa mvua utakoma.
Kutokana na mfumuko wa joto, gesi na hewa chafu, kutaifanya ardhi kuungua na kupoteza uhai wake na hatimaye kupata mipasuko na hivyo kuruhusu ujiuji (magma) utokao kwenye mwamba mgumu wenye joto kali la kuunguza kutoka chini ya ardhi na kupanda juu. Hali hiyo itasababisha hewa ya Oxygen kupotea na hivyo kuifanya ardhi ipoteze uhai wake na kupasuka vipande vipande.
Maji ambayo ni mchanganyiko wa hewa ya Hydrogen mbili na Oxygen moja (H2O) ambayo pia ni muhimu sana kwa maisha ya binadamu, nayo yatapoteza hewa ya Oxygen na hapo ndipo hewa ya Hydrogen itachanganyika na hewa ya carbon dioxed na kusababisha maji kupoteza sura yake ya kawaida na kuwa katika hali ya chembe chembe ndogo na kubwa.
Kuungana kwa hewa ya Carbon dioxed na ile ya Hydrogen na miale mikali ya jua itakayoshuka sambamba na gesi, itazikoleza hewa za Hydrogen na Carbon dioxed ambapo hali hiyo itazusha mlipuko mkubwa wa moto katika maji na hapo ndipo mfumo wa mambo ya kiulimwengu utakapotikiswa na kulipuka, bila shaka kutokana na hali hiyo, maisha ya binadamu na kila kiumbe hai yatafikia kikomo.
Wanazuoni wa kidini wakinukuu maandiko mbalimbali wanasema siku za mwisho wa dunia umri wa kuishi utapungua, dunia itajaa maasi, watu watazaa katika umri mdogo, matukio ya vita yatakuwa mengi, watu watapenda pesa na kadhalika. Je, hayo hayajatimia?
Basi ikiwa ni kweli, bila shaka itakuwa kweli yenye kutisha sana, je, wewe umejiandaa vipi kukabiliana na siku hiyo ngumu?

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa mitandao ya sayansi na mashirika ya habari. Mwandishi anapatikana kwa: 0754 28 30 01 E-mail: mussajr@yahoo.co.uk

MWISHO

Labels:

0 Comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA NDUGU

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home