Tuesday, December 23, 2008

Shamsa Mwangunga unawatania watanzania?

*mchezo wako unaweza kugeuka wa Barrick, North Mara.

Na Kachero Wetu, Mara


Wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa ameonyesha nia ya kupambana na vitendo vya ufisadi vilivyofanywa na viongozi wa Serikali iliyopita bado kuna mawaziri katika serikali yake wanaonekana kumkwamisha katika vita hivyo.

Wanaendeleza mazoea bila kujali cheo ni dhamana na ukipewa kitumie vizuri ili hata unaowatumikia waone umhimu wa wewe kuchaguliwa kuishika nafasi hiyo ambayo wengine wameikosa.

Waziri Shamsa Mwangunga ameonekana kuwa Miongoni mwa viongozi ambao hawajajua kuwa nchi ipo kwenye vita ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi ya Umma.

Waziri huyo aliyepandishwa kutoka Naibu katika Wizara ya maji Mwaka 2007 hadi kuwa Waziri kamili kwenye wizara nyeti ya Maliasili ambayo katika nchi zingine ndio tegemeo kuu la uchumi.

Wakati mwanamama huyo anachaguliwa kushika wadhifa huo alionekana mchapa kazi na kiongozi mwaminifu hadi akamvutia Rais Kikwete nakumpandisha cheo kuwa Waziri pale alipovunja Baraza la Mawaziri Aprili Mwaka 2008 nakuwatema mawaziri kadhaa.

Lakini kwa kipindi kifupi tu hiki alichokaa wizarani hapo waziri huyo amekwisha sahau wajibu wake wa kuwatumikia wananchi,ameanza kumsaliti Rais Kikwete kwa kwenda kinyume na serikali yake anamua kutumikia bwana mwingine ‘mwekezaji’

Ukweli huo unadhibitishwa na kitendo cha waziri huyo kusafiri kwenda Serengeti Mkoani Mara kwa mwaliko wa Kampuni moja ya kitalii ili akazindue barabara ya kilometa 13 iliyokarabatiwa kwa kifusi.

Tunataka Waziri huyo aeleze Umma wa watanzania kuwa alisafiri kwa gaharama za nani ,je alisafiri kwa gharama za kampuni hiyo huku akiwa ameongozana na ujumbe wa watu kadhaa kutoka wizarani kwake wakiwemo waandishi wa habari 13 au alisafiri kwa kodi za wananchi kwa ajili ya mambo binafsi .na aseme!.

Waziri Mwangunga kama angekuwa mwadilifu na kama angejua kuwa nchi kwa sasa inapambana na watu wanaotumia ofisi ya umma matumizi binafsi na tayari watu kadhaa wamekwisha pandishwa kizimbani kwa matumizi mabaya ya madaraka asingezubutu kwenda Serengeti.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba kampuni ya Mwekezezaji ya Grumet Reserve ambayo inamiliki Hoteli ya kifahari katika mbuga za Serengeti imekuwa ikilalamikiwa na wananchi wa Wilaya za Bunda na Serengeti kwa unyanyasaji wake unaokiuka misingi ya haki za binadamu.

Hata siku ile aliambiwa hadharani na wananchi wa Kijiji cha Mariwanda alipokwenda kufanya uzinduzi wa barabara ile,kutokana na unyanyasaji huo kampuni hiyo imekuwa na mahusiano mabaya kabisa na wananchi wa maeneo hayo kwa kutambua hilo imekuwa ikitafuta ukaribu wa kuwa na viongozi wa Serikali ili ipate pa kuegemea.

Lakini pia kama itadhibitika Waziri alisafirishwa na kampuni binafsi kwenda kuifanyia promo itakuwa ni kashfa nyingine inaodhibitisha pasiposhaka kuwa baadhi ya Viongozi wa Serikali ya Kikwete wamewekwa mfukoni na wawekezaji hivyo wamewatelekeza wananchi.

Aidha kama Waziri alitumia gharama za Serikali pia anapaswa kujiuzulu kwa kinachogomba hapa ni kwamba waziri anatoka Dar es Salaam, kwa gharama kubwa anakwenda kuzindua njia ya Km.13 iliyokarabatiwa kwa udongo na haijakamilika.

Kitu cha kushangaza nakuonyesha kuwa Waziri huyo ametumia vibaya madaraka yake au ameingizwa mkenge ni kwamba barabara hiyo nzima ina urefu wa Kilometa 28 kutoka Kijiji cha Balili Bunda hadi Mugeta kupita kandokando ya Mbuga kati ya hizo ni Kilometa 15 bado hazipitiki.

Kwa hiyo hata ukarabati wa Km 13 unadhibitisha kwamba barabara hiyo bado haijakamilika na kwasasa magari hayaitumii njia hiyo baadala yake wanatumia barabara ya Bunda Nyamuswa kwenda Isenye kupitia Mgeta badala ya Barabara iliyozinduliwa.

Kitu ambacho kimefichwa hapa ni kwamba barabara hiyo ilikarabatiwa kama kitu cha kusingizia ili waziri aweze kutembelea kampuni hiyo kwa madai ya kwenda kuzindua njia ya udongo yenye urefu wa Km13.

hata hivyo hoja hapa sio urefu wa barabara bali kinachoonekana kuwa ni kituko zaidi ni pale barabara hiyo ilipoonekana kukarabatiwa bila kuwekewa makaravati kwenye madaraja hali iliyofanya waziri aone aibu aseme kuwa wizara yake itatoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kununua makaravati.

Kama ukarabati ungekuwa umekamilika asingeahidi kutoa pesa za kununua makaravati hayo, lakini kingine kinachotia mashaka ni kwamba barabara hiyo imekarabatiwa kipande cha katikati pekee hadi kufikia kwenye kijiji chenye mgogoro ambapo waziri alienda kuhutubia wananchi.

Kufuatia kituko hicho wananchi wa eneo hilo walikerwa na hatua hiyo ya waziri kutumiwa na kampuni binafsi ili awakandamize wakazimika kumwambia kuwa toa hapa projo zako ,baadhi ya wandishi huru wa habari waliripoti tukio hilo.

Lakini haikuishia hapo wananchi walitaka waelezwe hatima yao na kampuni hiyo, itaendelea kuwanyanyasa na kuwachapa mijeledi mithiri ya wakoloni katika nchi yao, wanawake na watoto wanabakwa kukamatwa na kufungwa kwa kubambikiwa kesi pamoja na wao kuzuia kufanyakazi kwenye jirani na mbuga hiyo.

Baada ya kumuuliza maswali hayo huku wakiwa wamemwambia asiwapigie Projo aliwaomba wamsamehe aondoke kuwahi Dar es Salaam, kwani Ofisi yake ilikuwa imeungua ili mapema januari awapelekee majibu.

Swali Waziri Mwangunga alikuwa amekwenda ziara ya kiserikali Mara, kwa muda wa siku mbili au alikwenda kuitumikia kampuni binafsi kwa manufaa yake?

Habari zingine kutoka kwenye ziara hiyo zimebainisha kwamba kampuni hiyo ilitoa gari chakavu aina ya LandCruser kama jipya kwa Halmashauri ya Bunda ili litumike kwa ajili ya kudhibiti ujangili na waziri huyo akalipokea kama jipya.

Hapo ndio utata mwingine unapozuka kama kweli waziri huyo alikwenda ziara ya kiserikali au ya kuitangaza na kuboresha mahusiano ya kampuni hiyo kwasababu Serikali haiwezi kukabidhiwa gari chakavu na ikapokelewa kama jipya huku waziri akipiga makofi.

Kwa taarifa ni kwamba awali gari hilo lilikuwa likitumika kufanya shughuli za kawaida kwenye kampuni hiyo na wenyeji wanalifahamu na sasa wameamua kulitoa kwenye halmashauri ya Bunda kupitia mikono ya waziri ili kukamilisha ziara yake.

Kwa kuwa serikali ya kikwete imeanzisha vita dhidi ya ufisadi na watu viongozi wanaotumia vibaya madaraka yao ili kujilimbikizia mali ni matarajio ya umma kuwa katika siku za usoni watashuhudia mabadiliko katika wizara hiyo.

Hayo yatatokea ikiwa ziara ya waziri huyo itachunguzwa na kubainika sababu iliyomfanya aende Mara kwa muda wa siku mbili ,kwani hata wananchi walipotaka huduma kwake aliwaambia atarudi tena januaria kuwajibu maswali yao.

Hapo ndio maswali mengine yanapoibuka kuwa inamaana Waziri Mwangunga hakusikia amri ya Waziri Mkuu Pinda alipopiga marufuku semina na mikutano mbalimbali ili kubana matumizi ya Serikali .

Lakini wakati huohuo waziri anatunia gharama za walipa kodi kwenda Mkoani Mara nakushindwa kujibu Maswali tena anasema atatumia gharama zingine kwenda kujibu maswali yao kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Wananchi wanataka ukweli ubainike kama barabara hiyo isiyo hata na makaravati ndio ilimpeleke Waziri Mara au alikwenda kupokea zawadi yake hasa baada ya kuwa ameteuliwa kushika wadhifa huo? ziara hiyo isipochunguzwa na majibu kupatikana wananchi wanaweza kuasi nakufanya yale ya Mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya Barrick.







Labels: