Wednesday, November 21, 2007

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imeshindwa kutoa taarifa

Na Lucy Ngowi

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imeshindwa kutoa taarifa kama ilivyoahidiwa juzi na vyanzo vya habari kutokana na sababu mbalimbali.

Habari kutoka ndani ya wizara hiyo na Taasisi ya Mifupa na Tiba Muhimbili (MOI), zinasema kwamba sababu kubwa ya kutotolewa kwa ripoti hiyo ni kupitiwa kwa kina kabla kutolewa kwa jamii.

Mtoa habari huyo alisema kwamba ripoti hiyo ina mambo mazito na kwamba haiwezi kutolewa bila ya kupitiwa kwa kina ili kukwepa mkanganyiko unaoweza kujitokeza baadaye.

Sababu nyingine imeelezwa kwamba ni kutokuwako kwa waziri jijini Dar es Salaam, Profesa David Mwakyusa jana kwa kuwa alikuwa Arusha na leo anatarajiwa atakuwa jijini Dar es Salaam.

Jana gazeti hili liliripoti kuwa, Profesa Mwakyusa angeweka ripoti ya upasuaji tata inayoihusu taasisi ya MOI, ambayo mgonjwa aliyetarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa alifanyiwa upasuaji wa mguu, na yule aliyetarajia kufanyiwa upasuaji wa goti alifanyiwa wa kichwa.

Kwa mara ya kwanza tokea sakata hilo lilipotokea katika taasisi hiyo, uongozi wa juu umeruhusu kutolewa kwa taarifa mbalimbali zinazohusu wagonjwa hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Uhusiano Mwandamizi, Jumaa Almas alisema kuwa mgonjwa Emmanuel Didas anaendelea vizuri, ameanza kula peke yake, pia anaendelea na mazoezi.

Didas alipasuliwa kichwa badala ya mguu, Novemba Mosi mwaka huu na Emmanuel Mgaya alipasuliwa mguu badala ya kichwa, ambapo juzi Mgaya alifanyiwa upasuaji mwingine wa kichwa.

“Hali ya Didas inaendelea vizuri, ukimwambia kitu anaelewa lakini ule uwezo wake haujawa kikamilifu. Akiwa na shida anaweza kubonyeza kengele kuomba msaada. Ni kweli upande wake wa kulia umekosa nguvu,”alisema Almas.

Alisema hali ya Mgaya aliyefanyiwa upasuaji mkubwa, Jumatatu wiki hii bado si nzuri, yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

“Hali yake bado si nzuri haja improve vizuri. Hali hii ni kawaida kwa wagonjwa ambao wanafanyiwa upasuaji mkubwa. Vipimo vyake kutoka kwa madaktari wanaomtibu vinaonyesha kuna maendeleo tokea siku ile aliyofanyiwa upasuaji,”alisema Almas.

Hadi kufikia sasa madaktari wanne wameshasimamishwa kazi kutokana na upasuaji huo tata. Wawili kati yao walisimamishwa tu, mara baada ya tukio hilo kutokea, na wengine wawili wamesimamishwa juzi, baada ya kubainika kuwa walimwingiza Didas kinyemela kwenye chumba cha upasuaji bila kulipia.

Mwisho.